IQNA

Hamas yaafiki kubadilishana mateka na Israel kwa masharti

19:30 - April 10, 2020
Habari ID: 3472652
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema harakati hiyo imeazimia kuhakikisha kuwa mateka wa Kipalestina walioko katika vizuizi vya utawala wa Kizayuni wa Israel wanaachiwa huru katika mpango wa kubadilishana wafungwa na utawala huo ghasibu.

Ismail Haniya ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Mikhail Bogdanov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na kusisitiza kuwa, mpango huo wa kubadilishana mateka utafanyika tu iwapo utawala pandikizi wa Israel utakubali masharti ya harakati hiyo ya muqawama.

Hata hivyo Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina hajatoa maelezo juu ya masharti ya Hamas ya kukubali mpango huo wa kubadilishana wafungwa na utawala pandikizi wa Israel.

Kauli ya Haniya imekuja siku moja baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu kusema kuwa, utawala huo uko tayari kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas kuhusu suala la kubadilishana wafungwa. 

Hii ni katika hali ambayo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetahadharisha kuhusu hatari kubwa inayotishia uhai wa wafungwa karibu elfu tano wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika korokoro na jela za utawala haramu wa Israel kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa mujibu wa Shakir Ammarah, mwanachama mwandamizi wa Hamas, mateka Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel wako kwenye mazingira mabaya na ya kutisha yaliyoachanganyika na hofu ya maambukizo ya corona na akaongeza kwamba, utawala huo haujachukua hatua yoyote kuhusiana na suala hilo huku ukiendelea kupuuza miito ya kimataifa ya kuutaka uwaachie huru mateka hao.

Mwezi uliopita, Hamas iliziomba taasisi za kisheria za kimataifa zichukue hatua za kuwanusuru mateka wa Kipalestina katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kukithiri maambukizo ya virusi vya corona katika jela hizo.

Hivi sasa kuna mateka zaidi ya 5,700 wa Palestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel na miongoni mwao kuna wanawake 250 na watoto 47. 

Kuna wasi wasi wa kuenea ugonjwa hatari wa corona katika jela hizo zenye msongamano mkubwa. 

3890475

captcha