IQNA

Kiongozi wa HAMAS amtaka Mfalme wa Saudia awaachilie huru Wapalestina

22:01 - March 23, 2020
Habari ID: 3472596
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amemuandikia barua Mfalme Salman wa Saudia na kusitiza juu ya ulazima wa kuachiliwa huru haraka iwezekanavyo wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Saudi Arabia.

Katika barua yake, Ismail Hania amesema kuwa, kuachiliwa huru wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Saudi Arabia imekuwa ni dharura ya kibinadamu na kitaifa, hasa baada ya kuibuka virusi vya Corona ambavyo vinatishia uhai wa wafungwa hao.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Saudi Arabia inapaswa kuzingatia suala la ubinadamu na dini katika kuamiliana na faili la wafungwa wa Kipalestina.

Wakati huo huo, familia za Wapalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Saudi Arabia nazo zimetoa wito wa kuachiliwa huru ndugu zao na kusisitiza kwamba, tuhuma wanazokabiliwa nazo hazina msingi wowote.

Zaidi ya Wapalestina 60 wanashikiliwa katika magereza ya Saudi Arabia wakituhumiwa kuwa na uhusiana na  Harakati yaMapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Baadhi ya duru zinasema kuwa, raia wa Palestina waliokamatwa nchini Saudi Arabia na wanaoshikiliwa katika magereza ya nchi hiyo wanakabiliwa na mateso mbalimbali. Hayo yanajiri huku Saudia ikiendelea kukkosolewa kwa kukiuka haki za binadamu nchinii humo.

Hivi karibuni Bi Michelle Bachelet Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alieleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa kuendelea kukamatwa wapinzani wa serikali nchini Saudi Arabia hususan wanaharakati wanawake, sanjari na kukiukwa haki za binadamu.

3886966

captcha