IQNA

Ukombozi wa Palestina

HAMAS yakosoa kauli ya Katibu Mkuu wa UN dhidi wa wapigania ukombozi wa Palestina

21:17 - September 15, 2023
Habari ID: 3477602
TEHRAN (IQNA) Harakati ya Mapambano (Muqawama) ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imekosoa vikali kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ya kuyataka mapambano ya wapigania ukombozi Wapalestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kuwa eti ni "vurugu" na kusisitiza kwamba kinachofanyika katika ardhi za Palestina ni haki ya kujihami dhidi ya utawala unaokalia ardhi kwa mabavu.

Hamas imetoa kauli hiyo baada ya Guterres kusema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba hafikirii kama kwa kufanya kile alichokiita "vurugu na utumiaji nguvu", Wapalestina wataweza kutetea vyema maslahi yao.

Taarifa iliyotolewa na harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imesema: "Hamas inathibitisha kwamba jina potofu kama hilo haliambatani na haki halisi ya binadamu - yaani, haki ya kujihami dhidi ya uchokozi unaofanywa na utawala unaokalia ardhi kwa mabavu. Haki hii ya kujihami ni haki halali kwa mujibu wa sheria na kanuni za kimataifa.”

Hamas imesisitiza kwamba watu wa Palestina kamwe hawataifuta haki yao hiyo na wataendelea kupambana na uvamizi wa Israel na njama zake za Uyahudishaji hadi watakapoikomboa nchi yao.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina imebainisha kwamba uvamizi wa Israel na wa walowezi wa kikoloni na kifashisti ndio pekee unaopasa kuelezewa kwa kutumia maneno "vurugu" na "ugaidi", uvamizi ambao ndio unaohusika na  kuzidi kuchafuka kwa hali ya mambo, kuvuruga maisha ya watu wa Palestina na kuwanyima haki zao za kitaifa.

Taarifa ya Hamas imemalizia kwa kutoa wito kwa Guterres na Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu lao katika kuunga mkono haki za watu wa Palestina na piganio lao la haki kwa kulaani uvamizi wa Israel na uchokozi wake wa kila leo na kuwawajibisha viongozi wake kwa jinai na sera zao za kibaguzi ili kuwaruhusu Wapalestina watumie haki zao za kuwa huru na kujitawala katika ardhi yao ya asili.

4169047

Habari zinazohusiana
Kishikizo: hamas palestina israel
captcha