IQNA

Janga la corona

Mufti Mkuu Saudia: Swalini majumbani katika Mwezi wa Ramadhani

12:22 - April 18, 2020
Habari ID: 3472679
TEHRAN (IQNA) –Mufti Mkuu wa Saudi Arabia amesema sala zote katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ziswaliwe katika majumbani kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19 au corona.

Akijibu swali, Mufti Mkuu wa Saudi Arabia Sheikh Abdulaziz al-Sheikh alisema: “Hata sala ya Taraweeh inaweza kuswaliwa nyumbani kama haiwezekani kuswaliwa ndani ya msikiti kutokana na hatua zilizochukuliwa kuuzuia kuenea kirusi cha corona.” Aidha amesema Sala ya Eid ul Fitri nayo pia inaweza kuswaliwa nyumbani iwapo hali ya hivi sasa itaendelea.

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unatazamiwa kuanza tarehe 24 au 25 Aprili kwa kutegemea Mwezi Mwandamo.

Kati kati ya mwezi Machi Saudi Arabia ilipiga marufuku sala zote tano na sala za Ijumaa katika misikiti yote nchini humo ili kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19. Aidha Ibada ya Umrah imesimamsihwa kwa muda baada ya kufungwa Misikiti Miwili Mitakatifu ya Makka na Madina.

Hadi kufikia Aprili 18, idadi ya walioambukizwa COVID-19 nchini Saudi Arabia ilikuwa ni 7,142 huku waliofariki kutokana na ugonjwa huo wakiwa ni 87.

Saudi Arabia inatekeleza sheria ya kutotoka nje masaa 24 katika miji mikubwa na wanaotoka nje bila kibali maalumu wanafungwa jela au kutozwa faini.

3471174

captcha