IQNA

Saudi Arabia mbioni kuzuia kuenea corona Makka miongoni mwa vibarua wa kigeni

21:24 - April 14, 2020
Habari ID: 3472664
TEHRAN (IQNA) – Wakuu wa Saudi Arabia wako mbioni kuzuia kuenea ugonjwa wa corona au COVID-19 katika mji mtakatifu wa Makka kutokana na kuenea kwa kasi ugonjwa huo mjini humo pamoja na kuwa kunatekeleza sheria ya kutotoka nje kwa masaa 24.

Taarifa zinasema ugonjwa wa corona unaenea zaidi katika makazi yenye msongamano mkubwa katika mitaa ya mabanda na kambi za vibarua wa kigeni.

Hadi kufikia Jumatatu, mji wa Makka wenye idadi ya watu milioni mbili, ulikuwa na watu 1,050 walioambukizwa corona ikilinganishwa na mji mkuu wa Saudia Riyadh ambao wakati huo ulikuwa na wagonjwa 1,422 pamoja na kuwa ni mkubwa mara tatu zaidi ya Makka.

Idadi kubwa ya raia wa kigeni ambao hawajasajilia na pia msongamano mkubwa katika kambi za vibarua wa kigeni ni mambo ambayo  yamefanya iwe vigumu kudhibiti kuenea corona njini humo.

Mwezi Machi, wafanyakazi watano wa Shirika la Binladin, ambalo ni shirika kubwa zaidi la ujenzi Saudia, walippatikana na ugonjwa wa corona. Hali hiyo ilipelekea wakuu wa Saudia waweke karantini katika kambi ya wafanyakazi 8,000 wa shirika hilo na kusitisha kwa muda kazi za upanuzi wa Msikiti Mtakatifu wa Makka.

Kuhakikisha kuwa ugonjwa wa corona hauenei katika mji wa Makka ni muhimu kwa itibari ya ufalme wa Saudi Arabia ambao watawala wake wanajinadi kuwa ni wahudumu wa misikiti miwili mitakatifu ya Kiislamu katika miji ya Makka na Madina.

Hadi kufikia Aprili 14,  watu 5,369 walikuwa wameabukizwa corona Saudia na 73 wameaga dunia huku kukiwa na ripoti kuwa ufalme huo unaficha idadi halisi ya walioambukizwa na kufariki kutokana na ugonjwa huo hatari.

3891715/

captcha