IQNA

Waziri Mkuu Singapore: Ramadhani bado itakuwa na mvuto hata baada ya misikiti kufungwa

0:12 - April 23, 2020
Habari ID: 3472694
TEHRAN (IQNA) – Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong amesema ingawa misikiti imefungwa nchini humo, wanazuoni wa Kiislamu na waalamu wa dini watahakikisha kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani utaendelea kuwa na mvuto na maana yake halisi.

Akizungumza Jumanne, Lee alitangaza kuwa sheria za marufuku ya mijumuiko zitaendelea kutekelezwa hadi Juni 1 ili kuzuia kuenea ugonjwa wa corona.

Kwa msingi hiyo sheria hiyo itatekelezwa katika mwezi mzima wa Ramadhani ambao utaanza Aprili 24 au 25.

Lee aidha amesema amesikitika kuwa mwaka huu hataweza kupata fursa ya kujumuika na Waislamu katika misikiti wakati wa futari. Hatahivyo ameongeza kuwa: “Nimefahamishwa kuwa baraza la Kiislamu la Singapore, waalimu wa kidini na Waislamu kwa ujumla wanajitayarisha kuhakikisha kuwa mweziwa Ramadhani mwaka huu hautakuwa na mapungufu na utaendelea kuwa na faida.”

Amongeza kuwa kuna majukwaa mengi ya intaneti ambayo yatawaelekeza Waislamu kuhusu saumu ya Ramadhani, Zakat na misaada kwa wasijiweza.”

Lee halikadhalika amewapongeza Waislamu nchini Singapore kwa ushirikiano wao na kujitolea katika wakati huu mgumu wa janga la COVID-19.

Hadi kufikia Aprili 22, watu 10,141 walikuwa wameshaambukizwa corona au COVID-19 nchini Singapore huku wengine 12 wakifariki dunia.

Singapore au Singapuri ni nchi ndogo na iliyostawi katika Asia ya Kusini-Mashariki ambayo uchumi wake unategemea zaidi biashara, hasa benki pamoja na viwanda. Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia 15 ya watu wote milioni 5.6 katika nchi hiyo.

3471230

captcha