IQNA

Misikiti Singapore kufunguliwa kwa kuzingatia kanuni za afya

10:22 - May 28, 2020
Habari ID: 3472809
TEHRAN (IQNA)- Misikiti nchini Singapore itafunguliwa kuanzia Jumanne Juni pili kwa ajili ya swala zisizo za jamaa huku zuio la COVID-19 likianza kuondolewa nchini humo.

Huku Singapore ikianza kuondoa hatua kwa hatua zuio la COVID-19, Baraza la Kiislamu Singapore limesema duru ya kwanza ya kufunguliwa misikiti itafanyika kwa kuchukua tahadhari ya juu kabisa.

Baraza hilo linasema sheria kali za kiafya zitazingatiwa Ili kuzuia wimbi la pili la maambukizi jambo ambalo likijiri litapelekea misikiti ifungwe tena.

Kuanzia Juni 2-7, misikiti itafunguliwa kuanzia saa saba mchana hadi saa 12 jioni na itakuwa na maeneo matano maalumu ya swala na kila eneo linaweza kutumiwa na watu watano kwa wakati moja.

Baraza la Kiislamu Singapore limesema maeneo hayo ya swala yanaweza kutumiwa na kila mtu lakini kipaumbele ni kwa wale ambao kazi zao si za eneo maalumu kama vile madereva wa taxi na waendesha pikipiki.

Aidha wale wanaoweza kuswali nyumbani wamehimizwa kuendelea kufanya hivyo.  Hali kadhalika wazii, hasa wale wenye kinga dhaifu wametakiwa wajizuie kabisa kufika misikitini katika duru hii ya kwanza. Kuanzia juni 8 misikiti ya Singapore inatazamiwa kuanza sala tano za siku kwa jamaa na maeneo kuhusu taratibu zitakazofuatwa yatatolewa baadaye.

Singapore au Singapuri ni nchi ndogo na iliyostawi katika Asia ya Kusini-Mashariki ambayo uchumi wake unategemea zaidi biashara, hasa benki pamoja na viwanda. Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia 15 ya watu wote milioni 5.6.

3901625

captcha