IQNA

Ayatullah Qassim: Mapambano ya Kisiasa ya Wabahrain yanaendelea

11:44 - July 23, 2020
Habari ID: 3472990
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain Ayatullah Sheikh Isa Qassim amesema Wabahrain wataendeleza mapambano yao ya kisiasa hadi haki zao zitambuliwa na watawala wa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa wanaowanyima na kuwazuia wananchi wa Bahrain haki yao ya kulalamika ni watu wajeuri na wachokozi na akasisitiza kwamba, mapambano (muqawama) ya wananchi hao wa kukabiliana na utawala wa Aal Khalifa ungali unaendelea.

Sheikh Isa Qassim ameeleza katika taarifa kwamba, hakuna mtu yeyote anayeweza kudai kuwa hivi sasa wananchi wa Bahrain wanapata haki zao za kisiasa na akaongeza kuwa, jukumu sahihi na wajibu zilionao harakati za upinzani nchini humo ni kuendeleza muqawama wao mpaka hali iliyopo hivi sasa irekebishike.

Kiongozi huyo mashuhuri wa kidini nchini Bahrain amesema, licha ya kutokuwepo harakati zozote za utumiaji silaha dhidi ya utawala wa Aal Khalifa, lakini jela za Bahrain zimefurika wapinzani wa kisiasa huku mahakama za utawala huo zikiendelea kila mara kutoa hukumu za kidhalimu na kiuonevu.

Sheikh Isa Qassim amekumbusha pia kuwa, kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu, hukumu za kifo zinazotolewa dhidi ya wapinzani wa kisiasa zinategemea maelezo yanayotoloewa na washtakiwa wanaokiri makosa baada ya kuteswa kwa adhabu za aina mbalimbali ambazo mtu yeyote yule hawezi kuzihimili.

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiisamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

3911938

captcha