IQNA

Rais wa Uturuki: Mfumo wa kifedha wa Kiislamu unaweza kuiondoa dunia katika mgogoro

14:38 - June 15, 2020
Habari ID: 3472866
TEHRAN (IQNA)- Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema mfumo wa kifedha wa Kiislamu unaweza kutumika kuiondoa dunia katika mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na janga la COVID-19.

Erdogan alisema hayo jana Jumapili na kufafanua kuwa, "mfumo wa kifedha wa Kiislamu ndio ufunguo wa kuunusuru uchumi wa dunia unaoendelea kuvurugwa na janga la corona."

Rais wa Uturuki amesema hayo katika duru ya 12 la Kongamano la Kimataifa la Mfumo wa Kiislamu wa Kiuchumi na Kifedha ambapo pia amesema nchi yake inapania kuufanya mji wa Istanbul kuwa kitovu cha mfumo wa kifedha wa Kiislamu.

Amebainisha kuwa, "kinyume kabisa na yale yaliyoahidiwa, usambazaji wa mapato na utajiri unazidi kuharibika kote duniani, huku mwanya baina ya nchi na nchi ukizidi kupanuka."

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameeleza bayana kuwa, kupoteza maisha watu 440,000 kwa corona hakuwezi kuhusishwa tu na ugonjwa huo, lakini kumetokana pia na mifumo mibaya ya uchumi katika nchi mbali mbali duniani, ambayo inalinda tu matajiri na wenye nguvu.

Amesema, "katika baadhi ya nchi, watu ambao hawakuwa na bima ya afya waliachwa wafe. Hata nchi zilizostawi kiuchumi zilishindwa kuwapa wananchi wao barakoa na huduma za afya za kiwango cha chini." 

/3471697

captcha