IQNA

14:28 - June 23, 2020
News ID: 3472890
TEHRAN (IQNA) - Ufalme wa Saudi Arabia umetangaza rasmi kwamba ibada ya Hija mwaka huu itatekelezwa na watu wachache sana ambao ni raia na wakazi wa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imesema kuwa, Hija ya mwaka huu itashirikisha idadi ndogo ya mahujaji ambao ni raia wa Saudia na raia wa kigeni ambao ni wakazi wa nchi hiyo. Hatua hiyo ya kuwazuia mahujaji kutoka nje ya Saudia imechukuliwa kutokana na kuendelea maambukizi ya ogonjwa wa COVID-19 ambao haujapatiwa chanjo wala dawa.

Mwezi Machi mwaka huu pia Saudi Arabia ilisimamisha ibada ya Umrah kwa Waislamu kutokana na maambukizi ya virusi vya corona. Wakati huo Wizara ya Hija na Umra iliwataka Waislamu kote duniani kusubiri kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kujitayarisha kwa ajili ya ibada ya Hija.

Uamuzi wa Saudi Arabia wa kusimamisha ibada ya Hija mwaka huu umewavunja moyo mamilioni ya Waislamu kote duniani ambao huwekeza kwa miaka mingi kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo na kutimiza moja ya ibada muhimu za Kiislamu.

Mwaka jana karibu Waislamu milioni mbili na nusu walitekeleza ibada ya Hija huko Saudi Arabia.

Zaidi ya watu laki moja na sitini na moja elfu wameambukizwa virusi vya corona nchini Saudi Arabia na 1,307 miongoni mwao wameaga dunia.

3906343

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: