Mashirika ya serikali na sekta binafsi yanashirikiana kutekeleza na kuboresha mipango ya uendeshaji ili kuhakikisha kwamba waumini watafanya ibada ya Hija kwa urahisi na bila matatizo yoyote ndani na nje ya mji mtakatifu wa Mecca.
Mashirika yenye uwezo yanatazamia idadi kubwa ya mahujaji mwaka huu kufuatia Waislamu wapatao milioni 30 kutoka ndani na nje ya nchi Saudia kushiriki katika ibada ya Hija ndogo ya Umrah katika Msikiti Mtakatifu wa Makka (Masjid al Haram) , eneo takatifu zaidi la Uislamu wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu.
Aidha Waislamu wapatao milioni 33 waliswali katika Msikiti wa Mtume (Al Masjid an Nabawi), mahali pa pili patakatifu pa Uislamu, mjini Madina wakati wa Ramadhani. Mwezi huo huo pia ulishuhudia kuwasili kwa abiria milioni 9 kwenye Uwanja wa Ndege wa Prince Mohammed bin Abdulaziz huko Madina. Mahujaji wengi huwa wanatembelea Madina kabla au baada ya Hija.
Mwaka huu, wafanyakazi 3,500 wa Wizara ya Hija ya Saudia wamepewa jukumu la kuwahudumia Mahujaji wanaowasili Madina, ambako idadi kubwa ya maeneo ya kihistoria ya Kiislamu yamefanyiwa ukarabati na kupatiwa waongoza watalii ili kupokea wageni.
Waislamu wapatao milioni 1.8 kutoka kote ulimwenguni walifanya Hajj mwaka jana, kuashiria kurudi kwa viwango vya kabla ya janga la korona kwa idadi. Saudi Arabia imeanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya Hija ya mwaka huu iliyopangwa mwezi ujao.
3488198