IQNA

Utawala wa Kizayuni wa Israel wanyakua ardhi zaidi za Palestina

22:09 - October 06, 2020
Habari ID: 3473235
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Kizayuni umeamua kujenga maelfu ya nyumba za walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina unazoendelea kupora huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni haujazuiwa na hatua ya nchi mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo pandikizi.

Wakuu wa nchi za Imarati na Bahrain walidai kuwa wameamua kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni ili utawala wa Kizayuni uakhirishe kupora ardhi zaidi ya Wapalestina, madai ambayo yalikanushwa hapo hapo na Wazayuni, muda mfupi tu baada ya kutolewa na viongozi wa nchi hizo mbili za Kiarabu.

Jana usiku waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitangaza kuwa, utawala wa Kizayuni utaanza kujenga nyumba 5,400 za Wazayuni kwenye ardhi za Wapalestina katika kipindi cha siku mbili zijazo.

Ofisi ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) hivi karibuni ilitoa ripoti na kusema kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020, utawala wa Kizayuni umeshavunja nyumba 506 za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi huku nyumba 134 zikiwa ni za Wapalestina wa Quds Mashariki.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unadai kwamba baadhi ya nyumba hizo hazikuwa na vibali vya ujenzi, nyengine zimevunjwa kutokana na utawala wa Kizayuni kuzipiga faini na kuzitolesha kodi kubwa kupindukia za kuhakikisha kwamba Wapalestina watashindwa kulipa ili upate kisingizio cha kuzibomoa.

Kwa mujibu wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ujenzi wa vitongoj vya walowezi wa Kizayuni ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya kiburi cha kudharau azimio hilo, unaendelea kupora ardhi za Wapalestina na unawavunjia nyumba zao na kujenga za walowezi wa Kizayuni ili kuvuruga muundo wa kijiografia wa maeneo ya Wapalestina ili kuyapa sura ya Kizayuni.

3927750

captcha