IQNA

Rais wa Algeria asema nchi yake kamwe haitaanzisha uhusiano wa kawaida na Israel

19:03 - September 21, 2020
Habari ID: 3473190
TEHRAN (IQNA) - Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesisitiza kuwa, nchi yake inapinga vikali hatua zozote zile zenye lengo la kuanzisha uhusiano na utawala vamizi wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Rais huyo wa Algeria amesema wazi kuwa, nchi yake katu haitakuwa sehemu ya makubaliano ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba, inakosoa vikali hatua ya mataifa ya Imarati na Bahrain ya kuamua kuanzisha uhusiano na Wazayuni maghasibu.

Rais Abdelmadjid Tebboune amesisitiza kwamba, Algeria iko pamoja na wananchi madhulumu wa Palestina hivyo haiwezi kuanzisha uhusiano na utawala huo ghasibu.

Nchi ya Qatar nayo imetangaza kuwa, inaunga mkono malengo ya wananchi wa Palestina ya kupigania ukombozi wa ardhi zao pamoja na haki zao zilizoporwa na kughusubiwa na utawala haramu wa Israel.

Nchini Kuwait nako, mirengo mbalimbali ya kisiasa ya nchi hiyo  imekanusha madai ya rais wa Marekani, Donald Trump aliyedai kuwa nchi hiyo nayo itajiunga karibuni hivi katika mkumbo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Jumanne iliyopita, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain walijipeleka kwa Donald Trump huko Marekani na kutia saini hati za kutangaza kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni tofauti kabisa na malengo ya wananchi wa Palestina.

Hadi hivi sasa ulimwengu mzima wa Kiislamu bali hata baadhi ya nchi zisizo za Waislamu, kama Afrika Kusini zinalaani kitendo hicho cha kisaliti cha Bahrain na UAE.

3478275/

captcha