IQNA

Mamia ya wanafunzi wahofiwa kutekwa nyaraka baada ya wanamgambo kuvamia shule

19:43 - December 13, 2020
Habari ID: 3473451
TEHRAN (IQNA) - Mamia ya wanafunzi wanahofiwa kutekwa nyara katika jimbo la Katsina nchini Nigeria baada ya shule moja ya sekondari ya wavulana kuvamiwa na watu wenye silaha.

Taarifa zaidi kutoka Nigeria zinasema kuwa, watu wenye silaha wameishambulia shule ya wavulana iliyopo eneo la Dankara, na kuwateka nyara mamia ya wanafunzi.

Taarifa za awali zinasema kuwa, wanafunzi 400 hawajulikani walipo baada ya shambulio hilo.

Polisi katika jimbo hilo wamethibitisha uvamizi huo katika mazungumzo na vyombo vya habari, lakini wanasema hawana taarifa kuhusu watekaji.

Msemaji wa polisi katika jimbo hilo Gambo Issa amesema kuwa, wanafunzi wengine 200 waliokuwa wametorokea maeneo ya misituni , wakati washambuliaji waliipoivamia shule yao wamepatikana.

Kulingana na msemaji huyo wa polisi , vikosi zaidi vya usalama vimepelekwa katika eneo la tukio ili kukabiliana na wanamgambo hao wenye silaha , na kuongeza kuwa bado wanawasaka.

Wanafunzi walioweza kurejea kutoka mafichoni walielezea wasi wasi mkubwa uliotanda wakati washambuliaji walipoivamia shule yao.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema waliwaona washambuliaji wakiwateka nyara wanafunzi na kuondoka nao.

Mwanaume mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe amewaambia waandishi wa habari kwamba,  "Mtu mwenye silaha alipita mbele yangu na kufyatua risasi na akaingia ndani ya shule na kuwateka wanafunzi kadhaa. Tangu jioni tulipata taarifa kwamba watafanya shambulio na tukawaambia maafisa wa usalama lakini hakuna hatua iliyochukuliwa. "

Shambulio kama hilo lilitokea dhidi ya wasichana wa shule ya sekondari ya Chibok miaka sita iliyopita.

3473392

Kishikizo: nigeria wanamgambo
captcha