IQNA

Rais Rouhani

Imam Khomeini MA aliamini kwamba nguvu hasa ni za wananchi

23:07 - February 01, 2021
Habari ID: 3473611
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaonesha walimwengu rasilimali ya kijamii ya Iran.

Rais Rouhani amesema hayo leo wakati viongozi wa serikali walipokwenda kwenye Haram ya Imam Khomeini MA kusini mwa Tehran kwa ajili ya kutangaza utiifu wao kwa malengo matukufu ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka wa 42 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Amesema, katika mapinduzi na harakati nyingi duniani, kawaida viongozi wa mapinduzi na harakati hizo hutegemea nguvu za kijeshi au za vyama vya kisiasa. Hata hivyo amesema, Imam Khomeini MA aliamini kwamba nguvu hasa ni za wananchi na alifanya juhudi za kuwaamsha na kuwavutia wananchi kuingia katika njia ambayo aliichagua kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile ameashiria vikwazo na matatizo yanayotokana na janga la COVID-19 nchini Iran na kusema, serikali yake kwa kushirikiana na wananchi imefanikiwa kuvivunja nguvu vikwazo vya kidhalimu vya Marekani na imefanikiwa vizuri pia katika kudhibiti maambukizi ya kirusi cha corona.

Miaka 42 iliyopita tarehe Mosi Februari 1979, Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alirejea nchini Iran baada ya kuwa ubaidishoni kwa muda wa miaka 15. Kuingia kwake Imam Khomeini nchini Iran kuliharakisha kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya siku 10 baadaye yaani tarehe 11 Februari 1979. Sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran zinajulikana kwa jina maarufu la Bahman 22. Sherehe hizo mwaka huu zinafanyika tofauti ya miaka ya huko nyuma kutokana na maambukizi ya kirusi cha corona.

3473866

captcha