IQNA

Magaidi waua watu waumini 12 katika hujuma ndani ya msikiti Ijumaa mjini Kabul

7:13 - May 15, 2021
Habari ID: 3473910
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua 12 wameuawa na wengine zaidi ya 15 wamejeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea ndani ya msikiti wa Haji Bakhshi ulioko kwenye eneo la Shakar Dara viungani mwa mji wa Kabul wakati waumini walipokuwa wako kwenye ibada ya Sala ya Ijumaa hapo jana.

Shambulio hilo limejiri katika siku ya pili ya usitishaji vita uliofikiwa kati ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban ili kuruhusu Waislamu nchini humo kusherehekea Sikukuu ya Idul-Fitri.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi ya Kabul Ferdaws Faramarz, mada za miripuko zilizotumiwa katika shambulio hilo zilikuwa zimetegwa mapema msikitini humo.

Faramarz amethibitisha kuwa, watu wasiopungua 12 akiwemo Imam wa msikiti Mufti Nu'man wameuawa na wengine 15 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la Ijumaa ambalo hadi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika.

Mufti Nu'man ni alimu mwenye misimamo iliyo dhidi ya kundi la kigaidi la Kiwahabi la DAESH (ISIS) na amewahi mara kadhaa kutoa hotuba dhidi ya Uwahabi na kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji.

Imeelezwa kwamba kuna uwezekano idadi ya vifo vya shambulio hilo ikaongezeka, 

Shambulio hilo la kigaidi ndani ya msikiti wa Ijumaa mjini Kabul limetokea siku moja baada ya watu wengine wasiopungua 11 kuuawa katika matukio manne tofauti yaliyojiri sehemu mbalimbali nchini Afghanistan na kuvuruga utulivu wa kiwango fulani uliokuwa umetamalaki kufuatia usitishaji mapigano uliofikiwa kati ya serikali na kundi la Taliban.

Ijapokuwa hakujaripotiwa makabiliano ya ana kwa kati ya pande hizo mbili kutokana na kila upande kuendelea kuheshimu usitishaji huo vita wa muda, lakini mabomu ya kutegwa kandokando ya barabara yameendelea kusababisha maafa kwa raia nchini humo.

3971505

captcha