IQNA

Mamlaka ya Ndani ya Palestina inashirikiana na Israel kuwakandamiza Wapalestina

22:14 - June 27, 2021
Habari ID: 3474048
TEHRAN (IQNA)- Kuuawa shahidi mwanaharakati wa Kipalestina Nizar Banat mwenye umri wa miaka 42 na askari wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kumeongeza mashinikizo dhidi ya mamlaka hiyo na mkuu wake Mahmoud Abbas, ambapo sasa Wapalestina wanataka malaka hiyo ivunjwe na Rais Mahmoud Abbas ajiuzulu.

Wapalestina wamepitia wakati mgumu katika siku za karibuni. Jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi yao hazina mwisho ambapo hivi karibuni askari wa utawala huo tarehe 25 Juni waliwashambulia waandamanaji wanaopinga ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika mji wa Nablos ulioko katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na kujeruhi zaidi ya Wapalestina 400. Bila shaka hilo sio jambo la kushangaza kwa sababu utumiaji mabavu na ukatili ni katika dhati na utambulisho wa utawala huo ghasibu. Jambo la kushangaza ni siasa ambazo zimekuwa zikitekelezwa karibuni na Mamlaka ya Ndan ya Palestina dhidi ya raia wa Kipalestina na hasa wale wanaozuiliwa katika jela za mamlaka hiyo.

Nizar Banat ni miongoni mwa raia hao ambao wamepoteza maisha wakiwa mikononi mwa polisi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Banat alikuwa mwanaharakati wa kisiasa ambaye alipinga vikali kuhuishwa uhusiano wa malaka hiyo na utawala haramu wa Isreal. Kabla ya hapo mwanaharakati huyo alikamatwa mara kadhaa na polisi ya Malaka ya Ndani ya Palestina na kufungwa jela kutokana na upinzani wake dhidi ya suala hilo. Jambo muhimu hapa ni kuwa ukandamizaji na mabavu ya malaka hiyo ya Palestina hayaishii tu kwa Nizar Banat bali katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekamata na kuwaua shahidi Wapalestina wengine 15 wakiwemo wale wanaoshikiliwa katika jela zake.

Inavyoonekana ni kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeamua kuwafuta kabisa wapinzani wake katika uwanja wa kisiasa  wa Palestina na vile vile makundi ya mapambano ya Kiislamu. Daima kumekuwepo na hitilafu kati ya makundi hayo na Mamlaka ya Ndani ya Palestina, jambo ambalo limeipelekea mamlaka hiyo kufutilia mbali uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa kufanyika katika ardhi za Palestina. Suala jingine ni kuwa hata katika vita vya siku 12 vya utawala haramu wa Israel dhidi ya makundi ya mapambano katika Ukanda wa Gaza, Mamlaka ya Ndani ya Palestina haikuchukua hatua yoyote kuyasaidia makundi hayo dhidi ya adui wao wa pamoja bali ilikuwa na wasi wasi kuhusu kuongezeka nguvu za kijeshi za makundi hayo. Katika uwanja huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, imesema kuwa kuuawa shahidi Nizar Banat, ni dalili ya wazi kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeamua kulipiza kisasi dhidi ya wanamapambano kupitia mauaji na umwagaji damu.

Nukta nyingine ni kuwa ushahidi wa kuaminika unaonyesha kwamba Nizar Banat aliuawa kwa makusudi. Kuhusu hilo shirika huru la kuteteta haki za binadamu la al-Haq limesema matokeo ya vipimo vya madaktari yanaonyesha kuwa Nizar Banat aliuawa baada ya kuteswa na kwamba hakufa kifo cha kawaida. Alikuwa mpinzani mkali wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambaye alikuwa mgombea wa chama cha al-Hurriyya wal Karama katika uchaguzi mkuu wa bunge uliofutwa na ambaye karibuni pia alikuwa ameutaka Umoja wa Ulaya ufutilie mbali misaada ya kifedha kwa mamlaka hiyo kutokana na hatua yake ya kuakhirisha uchaguzi bila sababu yoyote ya maana. Alisema Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilikuwa imeamua kuhataraisha na kusaliti maslahi ya kitaifa ya Palestina kwa ajili ya kudhamini maslahi yake binafsi.

3980448

Kishikizo: palestina
captcha