IQNA

Kadhia ya Palestina

Mufti wa Oman alaani wanaotaka Kudhoofisha Muqawama wa Wapalestina

16:42 - December 09, 2023
Habari ID: 3478014
IQNA - Mufti Mkuu wa Oman amewakosoa wale wanaojaribu kudhoofisha harakati za mapambano ya Kiislamu (muqawama) za Wapalestina dhidi ya jinai za utawala haramu wa Israel.

Sheikh Ahmed bin Hamad Al Khalili aliwataka wanyamaze kimya na kuwaacha wapiganaji wa muqawama waendeleze mapambano ya kulinda ardhi na matukufu ya Palestina.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa X, Sheikh Al Khalili amelaani mauaji yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mwanazuoni huyo wa ngazi za juu zaidi nchini Oman amesema utawala ghasibu wa Israel unajichimbia kaburi kwa vita dhidi ya Gaza na kwa kufanya uhalifu wa kutisha.

Ukatili huu unaharakisha tu maangamizi ya Wazayuni, Sheikh Al Khalili alisisitiza. Vile vile alivikosoa vyama vinavyotusi na kutoa tuhuma dhidi ya wanamuqawama au wapigania ukombozi wa Palestina. Je, kuwalinda Waumini wanaume na wanawake wa Gaza, ambao haki zao zinakiukwa, si ni wajibu mtukufu kwa Ummah wote wa Kiislamu?

Kwingineko katika ujumbe wake, Mufti wa Oman amewapongeza wanamapambano wa Kiislamu wanaopigania ukombozi  wa Palestina kwa kuwatendea ubinadamu mateka wa Israel na wa kigeni, huku akiulaani utawala wa Kizayuni kwa kuwatesa wafungwa wa Kipalestina.

Tangu Oktoba 7 jeshi katili la Israel limeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 17,400 huko Gaza wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

3486336

Habari zinazohusiana
captcha