IQNA

Mkutano wa 2024 wa Umoja wa Kiislamu wamalizika kwa sisitizo la umoja ili kukomesha ukatili wa Israel

17:31 - September 22, 2024
Habari ID: 3479470
IQNA - Kongamano la 38 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu lilimalizika Jumamosi huku washiriki wakisisitiza umoja katika taarifa yao ya mwisho kama suluhu pekee la kusitisha ukatili wa Israel.

Mamia ya wanazuoni wa madhehebu ya Shia na Sunni walihudhuria Kongamano la 38 la Umoja wa Kiislamu lililoandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu katika mji mkuu wa Iran Tehran mnamo Septemba 19-21.

Katika taarifa ya mwisho, washiriki walieleza masikitiko yao juu ya hali mbaya iliyosababishwa na ukatili wa Israel katika Gaza iliyozingirwa na mashambulizi ya hivi karibuni huko Lebanon.

Aidha washiriki wamelaani utawala wa Israel kwa kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na mauaji ya raia. Halikadhalika wamelaani  juhudi za kuutambua rasmi utawala haramu wa Israel kwa kuanzisha uhusiano nao.

Taarifa hiyo imeitaja Quds tukufu au Jerusalem kuwa ni thamani kuu ya pamoja na suala la kuunganisha a ulimwengu wa Kiislamu na kusema: "Ulinzi wa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina unaozingatia misingi ya kidini ni miongoni mwa masuala ya lazima na ya kimaadili katika Uislamu."

Wanazuoni hao wa Kiislamu wameipongeza operesheni ya Kimbunga cha  al-Aqsa ya Oktoba 7 iliyotekelezwa na wapigania ukombozi wa Palestina na kuitaja kuwa ni jibu madhubuti na la kisheria kwa uvamizi na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel kwa zaidi ya miongo saba.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, ulinzi wa nchi za Kiislamu kwa ajili ya ardhi zao kwa ajili ya kukabiliana na ukatili na ujio wa utawala ghasibu wa Israel ni haki ya kisheria kwa madola yote ya Kiislamu.

Sehemu ya taarifa hiyo imesema: "Njia pekee ya kusimamisha jinai hizo za utawala ghasibu wa Israel ni umoja wa Umma wa Kiislamu na kuchukua hatua za kivitendo katika kukabiliana na utawala huo ghasibu."

Wanazuoni wa Kiislamu pia waliwasifu mashahidi wa muqawama na kulaani kama "uoga" mauaji ya viongozi na makamanda wa muqawama.

Kongamano la 38 la Umoja wa Kiislamu limefanyika chini ya kaulimbiu ya, "Ushirikiano wa Kiislamu ili kufikia Maadili ya Pamoja kwa Kusisitiza Suala la Palestina," na kwa mnasaba wa Maulidi au maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa  Mtume Mohammad (SAW).

Zaidi ya viongozi 200 mashuhuri wa kidini kutoka kote Iran na nchi za Kiislamu walihudhuria hafla hiyo ya siku tatu ili kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya hivi punde katika ulimwengu wa Uislamu, huku suala la Palestina likisalia kuwa kitovu cha mijadala hiyo.

/3489984

Habari zinazohusiana
captcha