IQNA

Nasrallah: Harakati ya Hizbullah ina taathira kubwa kieneo na Lebanon

16:38 - August 14, 2021
Habari ID: 3474188
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, kwa sasa harakati ya Hizbullah ni nembo kubwa ya muqawama na ina taathira ya kustaajabisha kitaifa na pia kikanda.

Sayyid Hassan Nasrallah ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni katika usiku wa kuamkia mwezi tano Muharram katika eneo la Dhaahiyah kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, ambapo sambamba na kuashiria matukio ya historia na ushujaa wa Imam Hussein (as) katika njia ya mapambano dhidi ya batili amesema: katika hali ya sasa na kwa kuzingatia vigezo vyote, hapana shaka Hizbullah ndicho chama kikubwa zaidi ndani ya Lebanon, jambo linachokifanya chama hiki kiwe na masuulia zaidi pia.

Nasrallah ameongezea kusema: "kila shakhsia wa kisiasa au alimu wa dini asiye na mfungamano na yeyote anapomshambulia au kumtuhumu mtu au kundi lolote, ajue kwamba anachokifanya kitakuwa na athari kwa hatima ya watu hivi sasa na siku za usoni; kwa hiyo jukumu na masuulia ya kila mmoja wetu kuhusiana na mienendo yetu ni hasasi na makubwa mno."

Itakumbukwa kuwa baada ya shambulio la maroketi la Hizbullah lililofanywa kujibu mashambulio ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel kusini mwa Lebanon, Bishara Butros Ar-Rai, kiongozi wa Wakristo wa Maroni nchini Lebanon alitoa matamshi dhidi ya Hizbullah na kulitaka jeshi la Lebanon lichukue hatua kuidhibiti harakati hiyo. Matamshi hayo ya Ar-Rai yaliwaudhi waungaji mkono wa muqawama nchini Lebanon na athari zake kushuhudiwa pia kwenye mitandao ya kijamii.

Alkhamisi ya tarehe 4 Agosti, kwa mara ya kwanza tangu vita vya siku 33 vya mwaka 2006, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia maeneo kadhaa ya kusini mwa Lebanon.

Na siku iliyofuata ya Ijumaa, harakati ya muqawama ya Hizbullah ikajibu mapigo kwa kushambulia kwa makumi ya makombora maeneo kadhaa ya kaskazini ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ambayo imepachikwa jina la Israel.

3990502

captcha