IQNA

Nasrallah: Tumejiandaa muda wote, na tuna uhakika wa kupata ushindi katika vita vyovyote

20:55 - August 08, 2021
Habari ID: 3474170
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema harakati hiyo ya muqawama haitaki vita, lakini pia haigopi vita kwa kuwa ina uhakika wa kuibuka mshindi iwapo vitaibuka.

Sayyid Hassan Nasrallah alisema hayo jana Jumamosi katika hotuba iliyorushwa hewani kwa njia ya televisheni, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya ushindi wa mrengo huo wa muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, katika vita vya kichokozi vya siku 33 vilivyoanzishwa na Tel Aviv dhidi ya Lebanon mwaka 2006.

Sayyid Nasrallah ameashiria uchokozi wa siku ya Alkhamisi uliofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na kueleza bayana kuwa, harakati hiyo huku ikiwa imejizatiti kwa zana za kisasa za kivita, imejiandaa barabara kutoa jibu zito kwa chokochoko za maadui.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, "tumejiandaa muda wote, na tuna uhakika wa kupata ushindi katika vita vyovyote. Jibu la Ijumaa ni sehemu ndogo ya uwezo wa kujihami Hizbullah. Tuna machaguo mengi na mbinu tofauti za kujilinda, kwa hiyo utawala wa Kizayuni ukifanya kitendo chochote cha kipuuzi, utakabiliwa na jibu zito."

Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah juzi Ijumaa ilitoa taarifa maalum na kutangaza kuwa, katika kujibu mashambulio ya anga yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel alfajiri ya kuamkia Alkhamisi katika sehemu za wazi za maeneo ya Al Jurmuq na Ash-Shawaakir, juzi asubuhi mnamo saa tano na robo kwa saa za Lebanon brigedi za shahidi Ali Kamil Muhsin na shahidi Muhammad Qassim Tahan za muqawama wa Kiislamu zilishambulia kwa makumi ya makombora ya milimita 122 ardhi zilizo jirani na kituo cha kijeshi cha Wazayuni maghasibu katika mashamba ya Shab'a.

Kadhalika Sayyid Nasrallah ameuonya vikali utawala haramu wa Israel dhidi ya kuwashambulia wakulima na raia wa kawaida huko kaskazini mwa Palestina na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni mashambulio yake yatadhoofisha harakati za muqawa, lakini ukweli ni kuwa, makundi hayo ya mapambano ya Kiislamu hivi sasa yamejiimarisha zaidi kiulinzi na kuboresha makombora yake.

3475452

captcha