IQNA

Kiongozi Muadhamu: Kutoa ufafanuzi na kueleza haki kunazima propaganda za adui

20:58 - September 27, 2021
Habari ID: 3474348
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia hujuma za kipropaganda zinazofanywa na maadui dhidi ya taifa la Iran kwa ajili ya kushawishi fikra za watu kwa kutumia mbinu na nyenzo mbalimbali na kusema harakati za kutoa ufafanuzi na kueleza haki zinazima hujuma hizo za kipropaganda.

Ayatullah Ali Khamenei ambaye leo ameuhutubia kwa njia ya video hadhara ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokusanyika kwa ajili ya kumbukumbua ya Siku ya Arubaini ya Imam Hussein, amesema kuwa kipindi cha kuanzia Ashura hadi siku ya Arubaini baada ya mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein bin Ali AS, ni miongoni mwa vipindi muhimu sana katika historia ya Uislamu na kuongeza kuwa, kama siku ya Ashura ilikuwa kilele cha jihadi ya kusabilia nafsi takatifu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kipindi cha siku arubaini baada ya mauaji hayo kilikuwa kilele cha jihadi ya kubainisha na kufichua haki na kweli; na kazi hii iliyofanywa na Imam Sajjad, Bibi Zainab na Ummu Kulthum na vilevile subira isiyo na kifani ya familia hiyo ya Mtume vilikamilisha jihadi kubwa na itakayobakia milele ya harakati ya Karbala.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hujuma kubwa ya kipropaganda ya maadui wa taifa la Iran kwa ajili ya kushawishi na kuathiri fikra za umma kwa kutumia mbinu na nyenzo mbalimbali na kusema kuwa, harakati ya kuweka wazi haki inabatilisha na kuzima hujuma hiyo ya propaganda. Ameongeza kuwa: "Nyinyi wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni matunda ya nyoyo za taifa na tumaini halisi la nchi hii, kila mmoja wenu anapaswa kuwa mithili ya taa inayomulika na kudhihirisha haki kwa kueleza na kubainisha ukweli." 

Vilevile amewataka kutumia suhula za mtandao wa intaneti na vyombo vya habari kwa ajili ya kujibu tuhuma mbalimbali na kusema kuwa, kigezo na msingi katika kazi ya jihadi ya kuweka wazi haki na kweli ni kutumia mbinu zinazoambatana na maadili na kueleza ukweli kwa kutumia mantiki, hekima na busara, sambamba na kujiepusha na matusi, tuhuma, ghilba. 

Ayatullah Khamenei ameeleza kufurahishwa na jinsi vijana walivyojizatiti kwa silaha ya fikra, mantiki na uelewa na kutilia mkazo udharura wa kudumishwa sifa hizo. Amesema kuwa, njia ya Bwana wa Mashahidi Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib ni njia yenye baraka inayomfikisha mwanadamu kwenye mafanikio.

4000633

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha