IQNA

Watu zaidi ya milioni 14 wameshiriki Arubaini ya Imam Husain AS huko Karbala, Iraq

20:50 - September 27, 2021
Habari ID: 3474347
TEHRAN (IQNA)- Wakuu wa mkoa wa Karbala nchini Iraq wamesema kuwa, takwimu za awali zinaonesha kwamba wafanya ziara ya Arubaini ya Imam Husain AS mwaka huu katika Haram ya mtukufu huyo ni zaidi ya watu milioni 14.

Kwa mujibu wa taarifa, idadi ya wafanya ziara ya Arubaini ya Imam Husain mwaka huu wa 1443 Hijria imepindukia watu milioni 14. 

Shirika la habari la Furat News limemnukuu Jassim al Fatlawi, Naibu Mkuu wa Mkoa wa Karbala huko Iraq akisema kwamba matayarisho ya kuwahudumia vilivyo wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS yalianza mapema zikiwemo huduma za kulinda usalama wao, usafiri, huduma za afya, vyakula, mahala mwa kupumzikia na huduma nyinginezo.

Wakati huo huo na sambamba na wiki ya pili ya programu maalumu ya usalama na huduma ya taasisi ya kujitolea ya wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi, Brigedia Jenerali Ali al Hamdani, kamanda wa operesheni wa kitengo cha al Furat al Awsat cha taasisi hiyo amesema, askari 9,500 wa al Hashd al Shaabi wanashiriki katika kulinda usalama wa wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS hivi sasa.

Katika upande mwingine, Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi jana usiku alitembea Karbala na kuonana ana kwa ana na makamanda wa kulinda usalama pamoja na maafisa wa kutoa huduma kwa wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS na kusisitiza kuwa,  kuwahudumia wafanyaziara hao ni wajibu mkubwa wa kimaadili, kibinadamu na kidini.

Maadhimisho siku ya Arubaini (Arobaini au Arbaeen) hufanyika kila mwaka tarehe 20 Safar, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, baada ya kupita siku Arobaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram, kwa ajili ya kukumbuka siku aliyouawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria Qamaria. Haram Takatifu ya Imam Hussein AS iko katika mji huo wa Karbala.

4000610

Kishikizo: arubaini ، karbala ، imam hussein as ، iraq
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha