IQNA

Tunisia kuhuisha hadhi ya Msikiti wa Al Zaytuna miongoni mwa Waislamu duniani

12:42 - December 07, 2021
Habari ID: 3474650
TEHRAN (IQNA)- Wakuu wa serikali ya Tunisia wametangaza azma ya kuinua hadhi ya Msikiti wa Al Zaytuna katika ulimwengu wa Kiislamu.

Masjid Al Zaytuna ni msikiti mkuu katika mji mkuu wa Tunisia na unaaminika kujengwa karne ya kwanza Hijria.

Wanahistoria wanadokeza kuwa, Msikiti huo ulijengwa mwaka 79 Hijria Qamaria sawa na 698 Miladia kwa amri ya Hissan ibn Nu’man na kukamilishwa na Ubaidullah ibn Habab.

Msikiti huo uko katika eneo lenye ukubwa wa mita mraba 5,000 na una milango tisa. Nguzo zake 184 ni zile ambazo zilitumika katika mji wa kale wa Carthage. Msikiti wa Zaytuna ni mkongwe zaidi katika eneo la kaskazini mwa Afrika (Maghreb) na kwa muda mrefu ulikuwa kitovu cha masomo ya Kiislamu kama vile Qur’ani na Fiqhi na pia lugha, historia na tiba. Chuo Kikuu cha Msikiti wa Zaytuna kilikuwa na moja ya vyuo vikuu vya kale zaidi ulimwenguni na idadi kubwa ya wanazuoni wa Kiislamu wamehitumu Al Zaytuna. Kati ya wasomi waliohitimu hapo ni mwanafalsafa na mwanahistoria maarufu Ibn Khaldun na malengo mashuhuri wa Tunisia Abul Qassim Ecebbi.

Hivi karibuni Waziri wa Masuala ya Kidini Tunisia Ibrahim Chaibu alisisitiza kuhusu kuhuisha hadi ya msikiti huo kama kitovu cha kidini na kielimu.

4018575

captcha