IQNA

Msikiti wa kwanza duniani uliochapishwa kwa 3D wafunguliwa Jeddah

21:26 - March 10, 2024
Habari ID: 3478484
IQNA – Msikiti wa kwanza duniani kujengwa kwa kutumia teknolojia ya uchapishaji ya 3D ulizinduliwa mjini Jeddah mapema mwezi Machi.

Msikiti huo uliopewa jina la marhum Abdulaziz Abdullah Sharbatly, uko katika kitongoji cha Al-Jawhara cha Jeddah na una ukubwa wa mita za mraba 5,600.

Msikiti huo wa aina yake umejengwa na Shirika Fursan Real Estate, likiongozwa na mfanyabiashara wa Saudi Wajnat Abdulwahed, kwa kutumia mashine za uchapishaji za  pande tatu yaani 3D za Guanli, shirika la  China linalomiliki teknolojia hiyo ya kisasa.

Mradi huo ni sehemu ya mradi wa Shirika la Kitaifa la Nyumba Saudia ulizinduliwa mbele ya viongozi wakuu wa serikali na wafanyabiashara.

Muundo wa msikiti huo unaonyesha urithi wa usanifu wa utamaduni wa Hejazi na umezingatia Kanuni ya Ujenzi wa Miji ya Mfalme Salman.

Ujenzi huo umelenga kuibua hali ya utulivu na umakinifu  miongoni mwa waumini.

Uzito wa jengo, mwanga wa asili, milango, na sehemu za mbele za nje ziliundwa kwa uangalifu ili kuboresha utambulisho wa msikiti. Minara imejengwa kwa namna ambayo itakuwa nembo ya mtaa huo. Eneo la wazi la nje limepata ilhamu kutoka eneo la Hijr Ismail karibu na Kaaba katika Msikiti Mkuu wa Makka, na litatumika  zaidi wakati msikiti una idadi kubwa ya waumini hasa wa sala ya Ijumaa, sala ya Tarawehe katika Mwezi wa Ramadhani, na Eid.

Abdulwahed, mjane wa Sharbatly na mkuu wa Shirika la Fursan Real Estate, alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo kwa kutumia teknolojia ya uchapishaji ya 3D ulikuwa mchakato mgumu na sahihi uliohitaji mbinu mpya ambazo ni tofauti na mbinu za jadi.

Alisema kuwa katika ujenzi walijitahidi kuzingatia asili usanifu majengo wa misikiti huku pia wakiibua  muundo wa kisasa. Aliongeza kuwa msikiti huo umejengwa heshima kwa marehemu mume wake.

Msikiti huo ni wa kwanza wa aina yake duniani kutumia teknolojia ya uchapishaji ya 3D, ambayo ni ubunifu unaoleta matumaini katika mustakabali wa usanifu majengo.

Kwa kuziba pengo kati ya mbinu za kale na uvumbuzi, msikiti wa kwanza duniani uliochapishwa kwa 3D huko Jeddah unaashiria hatua ya ujasiri kuelekea mustakabali endelevu zaidi na unaoendeshwa kiteknolojia.

Uchapishaji wa 3D huruhusu mifano ya digitali kubadilishwa vitu  kupitia michakato ya ziada ya utengenezaji.  Mfumo huu hupunguza ubadhirifu wakati wa ujenzi na pia kuongeza ufanisi katika sekta ya ujenzi.

Hadi miaka michache iliyopita, mbinu hii ya ujenzi kupitia uchapishaji wa 3D ilionekana kama hadithi ya kisayansi, lakini ni uhandisi ambao umechangia katika kuleta mapinduzi katika ujenzi na uzalishaji vitu mbali mbali duniani.

3487483

Kishikizo: msikiti teknolojia
captcha