IQNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ahutubu katika kikao cha OIC kuhusu Afghanistan

18:43 - December 19, 2021
Habari ID: 3474694
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: amani endelevu na ya kudumu itaweza kupatikana tu nchini Afghanistan ikiwa itaundwa serikali shirikishi na itakayojumuisha pande zote.

Hossein Amir-Abdollahian ametoa sisitizo hilo leo katika kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kilichofanyika mjini Islamabad, Pakistan.

Amefafanua kuwa, amani endelevu na uthabiti wa kisiasa na kijamii utaweza kupatikana nchini Afghanistan ikiwa tu utakuwepo ushirikishwaji wa watu wote na kuundwa serikali shirikishi na athirifu itakayotoa nafasi kwa makabila na madhehebu zote za nchi hiyo.

Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, kucheleweshwa kwa jambo hilo kutawapa fursa maadui wa Afghanistan ili sambamba na kushamirisha ugaidi wa Kidaesh, wawazidishie matatizo ya kiuchumi na hali mbaya ya maisha na ya kiafya watu wa nchi hiyo, kuwafanya washindwe kujikimu kwa mahitaji yao ya msingi ya maisha, kuustawisha upya mtandao mpana wa uhalifu wa kijamii na kuzidisha umasikini na baa la njaa baada ya miaka 20 ya nchi hiyo kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na kuteketezwa miundomsingi yake yiote na hivyo kuwafanya viongozi na watu wake washindwe kufanya chochote.

Katika hotuba yake hiyo kwa washiriki wa kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaitakidi kwamba, kuwepo amani endelevu na uthabiti wa kisiasa na kijamii ndani ya Afghanistan ni kwa manufaa ya pamoja ya eneo zima.

Halikadhalika amesema, kwa sababu za Kiislamu na kibinadamu, Iran itaendeleza misaada yake ya kibinadamu kwa watu wa Afghanistan.

662694

Kishikizo: oic afghani Abdollahian
captcha