IQNA

Waislamu duniani wakumbuka Kufa Shahidi Bibi Fatima Zahra AS

16:47 - January 05, 2022
Habari ID: 3474767
TEHRAN (IQNA) - Bibi Fatima Zahra SA binti mtukufu wa Bwana Mtume SAW na mwanamke bora duniani na akhera ni mwanamke ambaye ni kigezo na ruwaza njema na katika kipindi hiki Waislamu kote duniani wanakumbuka kufa shahidi mtukufu huyo.

Tarehe 3 Jamadi Thani mwaka wa 11 Hijria yaani ikiwa imepita miezi mitatu tu hivi tangu kufariki dunia Bwana Mtume SAW, ilikuwa ni siku ambayo Bibi Fatma Zahra AS alizidiwa na maradhi na huzuni kubwa kutokana na masaibu na mabalaa aliyokumbana nayo tangu alipoaga dunia baba yake kipenzi na kurejea kwa Mola wake. Kwa hakika hizi zilikuwa lahadha na nyakati za mwisho za umri uliojaa baraka wa binti huyu wa Bwana Mtume ambaye ni mke wa Imam Ali AS na mama wa Imam Hassan na Hussein AS. Huzuni na ghamu ya kuondokewa na baba yake kipenzi kwa upande mmoja, na masaibu aliyokumbana nayo baada ya kifo cha baba yake Mtukufu kwa upande wa pili, yalimlemaza kiafya na kumfanya ashindwe kuamka kutoka katika tandiko lake. Katika lahadha hizi za mwisho za maisha yake, kitu pekee kilichokuwa kikimpa utulivu ni ile ahadi ya Bwana Mtume SAW kwake wakati anaaga dunia ambapo alimwambia: Ewe binti yangu kipenzi! baada yangu wewe ndiye utakayekuwa mtu wa kwanza kutoka katika familia yangu ambaye atanifuata."

Fatima SA baada ya kufariki Mtume SAW

Katika masiku ya baada ya kufariki dunia baba yake, Bibi Fatima Zahra SA alikuwa na majukumu na masuuliya makubwa. Kwa hakika Fatima Zahra alikuwa mwanamke aliyejipamba kwa sifa za kipekee ambazo zilimtofautisha na wanawake na wanaume wote isipokuwa Mtume saw na Imam Ali bin Abi Twalib as. Mwanamke mwema huyu alijipamba na sifa zote njema na kufikia daraja ya juu ya uchaji Mungu. Mtume saw anasema:
"Kila mara Fatima alipokuwa akisimama katika mihrabu na mbele ya Mwenyezi Mungu, nuru yake ilikuwa ikiwaangazia Malaika mbinguni kama vile nuru ya nyota inavyowaangazia watu wa ardhini; na Mwenyezi Mungu husema: Enyi Malaika wangu mtazameni mja wangu Fatima, kiongozi wa waja wangu ambaye amesimama mbele yangu na mwili wake unatetemeka kwa khofu juu yangu na anafanya ibada kwa ajili yangu hali ya kuwa moyo wake umejaa khofu, unyenyekevu na khushui. Ninakushuhudisheni kwamba, nimewapa amani wafuasi wake kunako moto wa Jahanamu."

Baada ya kufariki mbora wa viumbe Bwana Mtume SAW, Bibi Fatima SA siku baada ya siku alikuwa akidhoofika. Imam Swadiq AS anasema kuwa, ghamu na huzuni ya kuondokewa na baba yake ilimzidi nguvu na kumlemea mwili wake. Jibril alikuwa akumjia na kumpa mkono wa pole kutokana na msiba wa kuondokewa na baba yake kipenzi na alikuwa akimpa khabari kuhusiana na baba yake, daraja na nafasi yake peponi na vile vile matukio ambayo yataikumba familia yake baada yam bora huyo wa viumbe kurejea kwa Mola wake. Imamu Ali as alikuwa akiandika kile alichokuwa akisikia kutoka kwa Jibril AS.

Lakabu ya Muhaditha

Aidha kabla ya hapo, Bibi Fatima as alikuwa akizungumza na Malaika na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akapewa lakabu ya Muhaditha. Imam Jaafar Swadiq AS anasema kuwa: Fatima as aliitwa Muhaditha kutokana na kuwa Malaika kutoka mbinguni walikuwa wakishuka na kuja kuzungumza naye kama ilivyokuwa kwa Mariam bint Imran.

Kwa hakika Fatima Zahra AS alikuwa mototo wa pekee wa Mtume wakati mbora huyo wa viumbe anaaga dunia na kurejea kwa Mola wake. Bibi Fatima alikufa shahidi na kuaga dunia akiwa na umri wa miaka 18 na akiwa ni mama asiye na mithili kwa watoto wanne. Kwa hakika binti huyu wa Mtume anajulikana katika historia ya Uislamu kuwa ni mwanamke wa kipekee, ruwaza na kiigizo chema ambaye aling'ara katika nyanja mbalimbali. Adhama na utukufu wa Bibi Fatima unadhihirika wazi katika riwaya na hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu watoharifu AS. Bibi Aisha mke wa Mtume SAW amepokea hadithi kutoka kwa Mtume SAW inayosema: Viongozi wa wanawake wa peponi ni wanne: Mariam bint Imran, Fatima bint Muhammad SAW, Khadija bint Khuwailid na Asia bint Muzahim mke wa Firauni.

Uchaji Mungu

Kwa upande wa ibada na uchaji Mungu, Bibi Fatima alikuwa amekwea na kufikia daraja ya juu kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu anamhutubu Mtume SAW akimwambia: Ewe Mtume SAW lau usingelikuweko wewe basi nisingeliumba ulimwengu, na kama Ali asingekuweko nisingekuumba wewe na kama Fatima asingekuweko basi nisingelikuumbeni nyinyi watu wawili."

Bibi Fatimah AS ni mwanamke anayezingatiwa kuwa ni mwanamke wa kutolea mfano katika dini ya Kiislamu, na pia ni kiigizo chema kwa kila mwanamke anayetafuta mafanikio katika maisha yake. Bibi Fatima binti Muhammad SAW ndiye mwanamke bora ulimwenguni aliyezaliwa na kupata malezi katika nyumba iliyokuwa ikishuka ndani yake Wahyi kutoka mbinguni.

Si hivyo tu, bali Bibi Fatima alihitimu mafunzo ya Uislamu katika madrasa ya Utume, na kutokana na mafunzo hayo aliweza kufikia daraja ya juu na tukufu. Katika kuthibitisha ubora wa Bibi Fatima, Mtume SAW amepata kusema, "Hakika Mwenyezi Mungu huwa radhi kwa kuridhia Fatimah, na huchukia kutokana na kuchukia kwa Fatima.

Mfano wa Utukufu

Kutokana na daraja kubwa aliyonayo Bibi Fatimah katika Umma wa Nabii Muhammad SAW imekuwa ni wajibu kwa kila mwanamke duniani kuiga mwenendo wa Bibi huyu katika maisha yake, ajing'arishe kwa nuru yake nzuri na afuate nyayo zake ambazo zitamuelekeza kwenye mafanikio na utukufu. Hakika Bibi Fatima SA, ni mfano wa kila utukufu na kila jema. Mwanamke yeyote atafanikiwa iwapo ataamua kufuata mwenendo wa Bibi Fatmah AS, na kinyume chake ni kuwa, kila mwanamke ataangamia iwapo ataamua kujichagulia mwenendo wake au kuiga usiyokuwa mwenendo wa Bibi Fatima AS.
Pamoja na adhama na utukufu wote huo, lakini msiba mkubwa wa baba yake pamoja na masaibu, maudhi aliyoyapata na dhulma aliyofanyiwa baada ya baba yake kufariki dunia ni mambo yaliyomvunja na kumtesa mno bibi Fatima AS. Muda mfupi baada ya baba yake kuaga dunia, alikumbana na maudhi na dhulma ya baadhi ya wale wanaodai kuwa ni Waislamu ambayo yalimfanya apoteze ujauzito wake na kubakia kitandani akiwa mgonjwa asiyejiweza.

Hatimaye Bibi huyo mwema ambaye kwa mujibu wa hadithi sahihi ya Mtume Muhammad SAW ni 'Mbora wa wanawake duniani' alikufa shahidi tarehe 3 Jamadi Thani kwa mujibu wa mapokezi ya baadhi ya wanahistoria akiwa na umri wa miaka 18 tu kwa mujibu wa nukuu mashuhuri zaidi. Aliswaliwa kwa siri na kundi dogo la waumini na kuzikwa usiku wa manane kwa mujibu wasia wake ambapo alitaka watu waliomdhulumu wasishuhudie jeneza na mazishi yake. Sala za salamu za Mwenyezi Mungu, Malaika, na Mitume wake zimshukie Bibi Fatima Zahra SA.

Amani iwe juu yako Ewe Fatma Zahra mwanamke bora wa duniani na Akhera, Bibi wa wanawake wa peponi, Mtukufu as-Sidiqah at-Tahirah Fatimatuz Zahra (Salaamullahi Alayha).

 

captcha