IQNA

Maandamano ya wanawake India kuunga mkono Hijab

21:22 - February 13, 2022
Habari ID: 3474924
TEHRAN (IQNA)- Huku mzozo wa Hijabu ukiendelea kutokota katika jimbo la Karnataka nchini India, wanawake Waislamu wameandamana katika mji wa Ludhiana, jimboni Punjab kuunga mkono haki ya kuvaa Hijabu.

Katika maadnamano hayo ya Jumamosi, wanawake hao wametaka haki yao ya kuvaa Hijabu ilindwe. Aidha wametangaza kupiunga hatua ya kupiga marufuku Hijabu katika shule na taasisi za kielimu jimboni Karnataka na wamesisitiza kuwa Hijabu ni chaguo binafsi.

Kushadidi kwa mizozo na hitilafu juu ya vazi la hijabu la wasichana na wanawake wa Kiislamu katika vyuo na taasisi za elimu katika jimbo la Karnataka huko kusini mwa India kumezusha hali ya wasiwasi na hofu kwa jamii za Waislamu nchini humo.

Kufuatia mzozo huo, mwanachuo mshichana Bibi Muskan Khan, mwenye umri wa miaka 19 wa India ambaye sasa anatambuliwa kuwa nembo ya mapambano ya kutetea vazi la hijabu, amesema anasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu shauri la uhuru wa vazi la hijabu na kusisitiza kuwa, Katiba ya India haipingi dini au dhehebu lolote.

Mzozo na hitilafu kuhusu vazi la hijabu katika vyuo vikuu na taasisi za elimu nchini India hususan katika jimbo la Karnataka ziliibuka baada ya wafuasi wa chama tawala chenye misimamo mikali ya Kihindu cha BJP wanaotumia skafu za rangi ya zafarani kama nembo ya chama chao kuwazuia wanachuo wanawake na wasichana wa Kiislamu kuhudhuria masomo kwenye vyuo vikuu au watupilie mbali vazi lao la hijabu.

Baada ya kupamba moto mzozo baina ya pande hizo mbili maafisa wa Chuo Kikuu cha Karnataka ambao walikuwa wakinyemelea fursa ya kupiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu, waliamua kupiga marufuku skafu za rangi ya zafarani na hijabu ya wanawake wa Kiislamu. Hii ni licha ya kwamba, Katiba ya India inaruhusu uvaaji wa vazi la hijabu, lakini inaonekana kuwa chama tawala cha BJP kimeamua kutumia mbinu mpya ya kukanyaga haki hiyo ya Waislamu. Kwanza chama hicho kiliwahamasisha wafuasi wake wenye misimamo mikali kuzusha tafrani na ghasia katika vyuo vikuu kuhusu vazi la hijabu  iliviburuta vyombo vya sheria hususan mahakama katika mzozo huo na kisha mahakama hizo zinazodhibitiwa na Wahindu wenye misimamo mikali, zitoe hukumu na maamuzi kwa maslahi ya wafuasi wa chama hicho. Mfano wa ukweli huo ni kadhia ya Msikiti wa kihistoria wa Babri.

Marufuku ya kuvaa hijabu iliyowekwa katika vyuo vya jimbo la Karnataka imeamsha wimbi la hasira za wanafunzi Waislamu, ambao wanasema, hiyo ni hujuma inayolenga imani yao ambayo inatambuliwa rasmi na katiba ya India, huku makundi ya Kihindu ya mrengo wa kulia yakitumia mabavu kuwazuia mabanati wa Kiislamu wasiingie vyuoni na hivyo kuibua mivutano ya kijamii jimboni humo.

Hapana shaka yoyote kwamba, kuingia Mahakama Kuu ya India katika mzozo wa vazi la hijabu kunaweza kudhibiti harakati na njama za makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka na kuzuia mizozo na machafuko ya kijamii. Hata hivyo inaonekama kuwa, nguvu kubwa ya chama tawala cha BJP inawawezesha wafuasi wenye misimamo mikali wa chama hicho kudhibiti taasisi muhimu na zinazochukua maamuzi ya juu.

3477794

Kishikizo: india waislamu hijabu
captcha