IQNA

Uchambuzi

Hali katika nchi za Kiislamu wakati wa Idul Fitr mwaka huu

16:19 - May 05, 2022
Habari ID: 3475210
TEHRAN (IQNA)- Nchi za Kiislamu zimesherehekea Idul Fitr baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wakati ambao katika baadhi ya nchi za Kiislamu amani na usalama inaonekana kuwa kiungo muhimu zaidi kinachokosekana katika maisha ya watu wa nchi hizo.

Kwa mfano tu, nchini Afghanistan, watu wa nchi hiyo wanasherehekea sikukuu ya Idul Fitr, ambayo imechanganya furaha na huzuni kutokana na milipuko iliyotokea wiki za hivi karibuni katika maeneo tofauti ya nchi hiyo, na familia nyingi zinaomboleza wapendwa wao. Hii ni licha ya kwamba, dini ya Uislamu ni dini ya amani na udugu; na mifarakano, chuki na uadui baina ya Waislamu si tu kwamba havifai kuwepo kabisa baina ya Waislamu, lakini pia vinazuia Umma wa Kiislamu kupiga hatua za maendelea na kutatua matatizo yao.

Weledi wa mambo wanasema maadui wa Uislamu siku zote wanajaribu kutumia tofauti zilizopo kati ya madhehebu za Kiislamu kupandikiza chuki, uhasama na mifarakano ili Waislamu daima washughulishwe na mambo yao ya ndani.

Ingawa kwa kiwango ulani, Waislamu katika nchi nyingi wamefanikiwa kuzima njama za maadui wa Uislamu kwa busara na hekima, watu wa nchi kama Afghanistan bado wanatamani kuona amani na usalama ili familia zijumuike pamoja kwa amani na kusherehekea sikukuu za Kiislamu kama hii ya sasa ya Idul Fitr. Kwa hivyo, sikukuu hii ni fursa adhimu kwa viongozi wa kisiasa na kidini wa nchi mbalimbali wakiwemo wa Afghanistan, wakiongozwa na mafundisho ya Uislamu, kufanya kazi ya kuimarisha umoja wa kitaifa na udugu baina ya makundi na madhehebu zote za Kiislamu, ili vizazi vijavyo visiathiriwe na kutumbukia katika fitina, hitilafu na mapigano ya ndani. 

Idul Fitr ni fursa adhimu ya kuimarisha misingi ya umoja, upendo na udugu katika nchi n jamii za Waislamu, na viongozi wa kidini na kisiasa katika nchi zinazokabiliwa na migogoro ya ndani wanaweza kufanya jitihada za kuimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu kwa kufuata maelekezo ya Qur'ani Tukufu na mafundisho na sira ya Mtume wetu Muhammad (saw), ili maadui wasiweze kutumia vibaya tofauti za kimitazamo kati madhehebu za Kiislamu.

Jambo hili muhimu litatimia wakati mafundisho ya Uislamu yatakapoondolewa katika hali ya kuwa nara na kauli mbiu tupu na badala yake yatekelezwe kivitendo.

213276

Kishikizo: idul fitr waislamu
captcha