IQNA

Fikra za Kiislamu

Kuwaenzi na kuwakirimu mayatima ni muhimu katika Imani zote

12:45 - August 25, 2022
Habari ID: 3475678
TEHRAN (IQNA) – Miongoni mwa masuala ambayo yana mizizi katika Fitra (asili) ya binadamu ni kuwasaidia na kuwaenzi watoto waliofiwa na wazazi wao.

Viongozi wa dini na wanazuoni wa dini zote wameweka mkazo katika kuwasaidia na kuwahudumia watoto yatima.

Katika kila jamii kuna watoto waliofiwa na wazazi wao kwa sababu tofauti na baadhi hupelekwa kwenye vituo vya watoto yatima ili kutunzwa

Lakini malazi, chakula na nguo sio vitu pekee ambavyo mayatima wanahitaji. Wanachohitaji zaidi ni wema na huruma kutoka kwa wengine.

Mwanadamu anahitaji upendo katika maisha yote, haswa katika utoto. Ikiwa watoto hawatapata huduma na uangalifu katika umri mdogo, hakuna uhakika kwamba watakuwa na maisha yenye afya ya kiakili. Watoto kama hao wanaweza kupatwa na matatizo ya kibinafsi na kijamii wanapokua kwa sababu ni katika familia ambapo mtu hulelewa kiroho, kijamii na kiamaadili kwa njia bora zaidi.

Moja ya masuala ambayo Uislamu unatilia mkazo mkubwa ni kuwaheshimu na kuwapenda watoto yatima. Imesimuliwa katika Hadith nyingi kwamba Mtukufu Mtume (SAW) alipomwona yatima, alitumia muda fulani kumlea mtoto huyo.

Qur’ani Tukufu pia inazungumzia suala hili na inakataza kuwanyanyasa au kuwakejeli mayatima: “Kwa hiyo msiwafanyie ukali mayatima.” (Aya 9 ya Sura Ad-Duhaa)

Pia inawataja mayatima kama kundi moja la watu wanaohitaji kusaidiwa kifedha kwa sababu kwa kawaida wanaishi katika umaskini baada ya kupoteza wazazi wao. “Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.” (Aya ya 177 ya Sura Al-Baqarah)

Kwa bahati mbaya, wapo wengine ambao sio tu kwamba wanakataa kuwasaidia mayatima bali hutumia hali zao na udhaifu wao na kunyakua mali zao. Qur’ani Tukufu imefananisha hili na kula moto:  Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni. (Aya ya 10 ya Sura An-Nisa)

captcha