IQNA

Fikra za Kiislamu

Kupenda anasa za kidunia ndio chanzo cha uchoyo na ulafi

22:42 - August 27, 2022
Habari ID: 3475690
TEHRAN (IQNA) - Kushikamana na anasa za kidunia na tama ya utajiri kunaweza kuzingatiwa kuwa chanzo cha madhambi mengi na hata matatizo ya kisaikolojia.

Qur’ani Tukufu katika aya nyingi inawaonya wanadamu dhidi ya kushikamana na mambo ya kidunia.

Mapenzi ya mambo ya kidunia yanapozuka katika nafsi ya mwanadamu na kumpeleka kwenye uchoyo, ulafi  na kutamani mambo ya kidunia, anaanza kutembea katika njia hiyo na kadiri anavyosogea kwenye njia hii, ndivyo anavyozidi kusahau njia sahihi.

Qur'ani Tukufu inakosoa udunia uliokithiri na kupenda mambo ya kidunia na inawaonya wanadamu waepuke kwa sababu vinginevyo, atakanyaga maadili yote ya kibinadamu na ya kiroho.

Katika aya kadhaa za Qur’ani, ulimwengu umeelezewa kama mchezo na pumbao:

“Na maisha ya dunia si chochte ila ni mchezo na pumbao tu. Na hakika nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wanao mcha Mungu. Basi, je, hamtii akilini? (Surah Al-An'am, Aya ya 32)

Katika aya nyingine inasema, " Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu kali na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu. (Surah Al-Hadid, Aya ya 20)

Kwa hakika Qur’ani inawafananisha wale wanaoipenda dunia na watoto wasiojua yanayowazunguka na wanacheza bila ya kuona hata hatari iliyo karibu nao.

Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani wanagawanya miaka arobaini ya mwanzo katika maisha ya mwanadamu katika vipindi vitano:

Anacheza katika miaka minane ya kwanza, kisha anahusika katika burudani na uzembe kwa miaka minane.

Anafuata urembo na mapambo kwa muda wa miaka minane, kisha anakaa miaka minane akiwa na kiburi na kujifakharisha na katika miaka minane ya mwisho anajikusanyia vitu vya kidunia.

Katika arobaini, utu na shakhsia (personality)  huwa imejikita na ni vigumu kubadilika hadi mwisho wa maisha yake. Kwa hivyo kwa wale wanaoipenda dunia hii, yamkini wasipate  fursa ya kufikiria maisha ya kiroho na maisha ya milele ya Akhera.

captcha