IQNA

Sura za Qur’ani Tukufu/ 15

Surah Al-Hijr; Uumbaji wa Mwanadamu na Mwanzo wa Uadui wa Shetani

21:33 - October 17, 2022
Habari ID: 3475945
TEHRAN (IQNA) - Kumekuwa na nadharia na mitazamo tofauti juu ya kuumbwa kwa mwanadamu, na mtazamo wa Uislamu juu ya hili umetajwa ndani ya Qur’ani ikiwemo katika Sura al Hijr.

Al-Hijr ni sura ya 15 ya Quran, Ina aya 99 na iko katika Juzuu ya  14 . Ikiwa ni sura ya Makki, ni sura ya 54 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Jina Hijr linatokana na kisa cha watu wa Mtume Saleh (AS) waliotajwa katika aya ya 80 hadi 84. Walijulikana kuwa watu wa Hijr kwa vile walikuwa wakiishi katika ardhi iitwayo Hijr. Saleh alikuwa nabii wa Bani Israeli na pia alikuwa kutoka dhuria au kizazi cha Nabii Nuh (AS). Jina lake limetajwa mara 9 katika Qur’ani Tukufu.

Surah Al-Hijr, miongoni mwa mada nyinginezo, inahusu mwanzo wa uumbaji wa ulimwengu, dalili za Ufufuo, imani kwa Mungu, umuhimu na adhama ya  Qur’ani Tukufu, na adhabu kwa wakosaji. Pia inahusu kisa cha kuumbwa kwa Hadhrat Adam (AS), kumsujudia Malaika na kukataa kwa Ibilisi kufanya hivyo, bishara njema ya Malaika kwa Nabii Ibrahim (AS), adhabu kwa watu wa Lut na hadithi ya watu wa Thamud.

Miongoni mwa masuala muhimu yaliyotajwa katika sura hii ni Aya kuhusu uumbaji. Katika Aya ya 26 hadi 43 hadithi ya kuumbwa wanaadamu na majini imesimuliwa. Imebainishwa pia kwamba Malaika walimtii Mungu na kumsujudia Adam (AS) huku Ibilisi akakataa kufanya hivyo na kwa hiyo, akafukuzwa peponi.

Hadithi ya kuumbwa kwa Adam (AS) na uasi wa Ibilisi na hatima yake ni onyo kwa wanadamu wote kwa sababu Ibilisi alifukuzwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kukataa kumsujudia mwanadamu lakini kabla ya kufukuzwa, alimuomba Mwenyezi Mungu amruhusu kuwapotosha wanadamu. Hili lilikubaliwa na Iblis akaapa kuwapoteza watu wote, isipokuwa waja wema wa Mwenyezi Mungu.

Hii haimaanishi kwamba mwanadamu hana budi kudanganywa na Shetani (Iblis). Katika Surah Al-Hijr, Mwenyezi Mungu anaonyesha njia mbili kwa mwanadamu kuchagua moja kulingana na hiari yake. Wengine huchagua njia sahihi na kukataa kumruhusu Shetani awadanganye. Hao ndio tunaowasoma katika aya ya 45 na 46 ya Sura  hii: “Wachamungu wataishi katika mabustani yenye mito. Na wataambiwa waingie humo kwa amani na salama.”

Wengine, kwa upande mwingine, wanamfuata Shetani. Katika hali hiyo, “Jahannamu ni mahali palipoahidiwa kwa ajili yao wote.” (Surah Al-Hijr, aya ya 43).

captcha