IQNA

Jibu kwa jinai za Marekani

Wamarekani zaidi wakabiliwa na vikwazo vya Iran

21:41 - November 01, 2022
Habari ID: 3476020
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa imeyaweka majina ya shakhsia kumi na taasisi nne za Marekani kwenye orodha yake ya vikwazo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza katika taarifa iliyotolewa Jumatatu usiku kuwa, imewawekea vikwazo shakhsia kumi wa Marekani na taasisi nne za nchi hiyo.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewawekea vikwazo shakhsia na taasisi zifuatazo kwa kuendesha harakati zilizo dhidi ya haki za binadamu, kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kueneza ghasia na fujo nchini Iran, kuchochea na kuhamasisha vitendo vya kigaidi, kukabiliana na juhudi na harakati za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na ugaidi na vilevile kuongeza mashinikizo dhidi ya taifa la Iran ambayo ni kielelezo cha ugaidi wa kiuchumi.

Hayo yanajiri wakati ambao, taarifa ya pamoja iliyotolewa na Wizara ya Intelijensia ya Iran na Shirika la Upelelezi la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imeweka wazi nafasi ya Marekani katika machafuko ya hivi karibuni hapa nchini.

Taarifa hiyo ya pamoja imesisitiza kuwa: Nyaraka zilizopo za kijasusi zinaonyesha kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa ushirikiano na mashirika ya kijasusi ya washirika na vibaraka wake, walipanga kuzusha machafuko na pia kutayarisha uwanja wa kuzidishwa mashinikizo ya kigeni dhidi ya Iran.

Taarifa za kiintelijensia zinaonesha kuwa, CIA imekuwa na ushirikiano wa karibu na Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Uingereza (MI6), shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD), Idara ya Ujasusi wa Kigeni wa Saudia na nchi nyingine kadhaa katika kutekeleza mpango huo. 

Miongoni mwa shakhsia wa Marekani waliomo kwenye orodha hiyo ya vikwazo ni Michael Kurilla, Kamanda wa Kamandi ya Kijeshi ya Kikanda ya Marekani (CENTCOM), Gregory Guillot, Naibu Kamanda wa CENTCOM, Juan Zarate, Mkurugenzi wa Kituo cha Nguvu za Kifedha na Kiuchumi katika Wakfu wa Kutetea Demokrasia na Taasisi ya American Enterprise na Mark Wallace, mkurugenzi mtendaji wa Muungano dhidi ya Iran ya Nyuklia.

Taasisi hiyo ya Muungano dhidi ya Iran ya Nyuklia, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Safu ya 9 ya Kikosi cha Anga cha Jeshi la Marekani na Kikosi cha Gadi ya Taifa ya Marekani ndizo taasisi nne zilizomo kwenye orodha ya vikwazo vya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.

Vikwazo walivyowekewa shakhsia hao na taasisi hizo za Marekani ni vya kuzuia utoaji viza na kuingia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuzuiliwa mali na milki zao katika eneo lililo chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzuiwa akaunti zao za benki katika mfumo wa fedha na benki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

4096028

captcha