IQNA

Wasomaji Qur'ani bingwa

Ustadh Mustafa Ghalwash akisoma aya za Sura al Baqarah katika Qur'ani Tukufu

13:40 - November 16, 2022
Habari ID: 3476096
TEHRAN (IQNA)- Klipu ya qiraa ya Qur'ani Tukufu ya qarii mashuhuri wa Misri marehemu Sheikh Ragheb Mustafa Ghalwash imesambazwa katika mitandao ya kijamii.

Katika klipu hii ya muongo wa 1990, Qarii huyu anasema aya za 142 na 143 za Sura al Baqarah zisemazo:

142: Wapumbani miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo nyooka. 143: Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu. 

Qiraa hii ilikuwa katika msikiti mmoja ulioko Tanta ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Gharbia wa Misri.

Sheikh Ragheb Mustafa Ghalwash  alizaliwa Julai 5 mwaka 1938 nchini Misri na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani. Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa tayari amehifadhi Qur'ani nzima katika rika la barobaro na kuanza kusoma kitabu hicho katika hafali na majlisi mbalimbali akiwa na umri wa miaka 16.

Alijiunga na Radio ya Qur'ani Misri ambapo alipata umashuhuri mkubwa wakati huo akisoma pamoja na magiwji wengine wa qiraa ya Qur'ani Tukufu kama vile Mustafa Ismail, Abdul Basit Abdul Samad, Mahmoud Khalil al-Husari na wengine.

Sheikh Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa miongoni mwa wasomaji wa Qur'ani waliofanya safari nchini Iran baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran. Qiraa na kisomo cha gwiji huyo wa Misri kilipendwa sana nchini Iran na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu.

Sheikh Ghalwash alitembelea Iran nyakati tafauti kuanzia mwaka 1989 hadi 2000 na katika moja ya safari zake hizo alipata fursa ya kusoma Qur’ani Tukufu katika kikao kilichohudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei.

Sheikh Ghalwash aliaga dunia Februari 4 mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 78 uliojaa baraka.

4032749

Kishikizo: qurani tukufu ghalwash
captcha