IQNA

Wanazuoni Mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiislamu/5

Valeria Porokhova na mojawapo ya tafsiri bora za Qur'ani katika Kirusi

14:56 - November 16, 2022
Habari ID: 3476097
TEHRAN (IQNA) -Valeria Porokhova ameandika mojawapo ya tafsiri bora zaidi za Qur'ani Tukufu katika lugha ya Kirusi.

Ubora wa tafsiri aliyoandika Porokhova umethibitishwa na vituo kadhaa vya Russia (Urusi) na pia Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri.

Valeria (Iman) Porokhova ni mwandishi wa Kirusi aliyezaliwa Mei 14, 1940 na kisha akapata taufiki ya kusilimu baad aya kufanya utafiti wa kina kuhusu Uislamu.

Alizaliwa katika familia ya Kikristo. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Moscow na kusoma tafsiri kadhaa za Kirusi za Qur'ani Tukufu wakati akiwa anaendelea na masomo. Akirejelea hisia aliyokuwa nayo baada ya kusoma Qur'ani Tukufu, alisema: “Nilihisi kana kwamba nilikuwa Mwislamu maishani mwangu. Niliposoma Qur'ani, nilipata majibu ya maswali mengi niliyokuwa nayo katika maisha yangu ingawa sikujua chochote kuhusu Uislamu.”

Baadaye aliolewa na mwanazuoni wa Kiislamu wa Syria ambaye alikuwa mwenyekiti wa kituo cha Kiislamu nchini Russia. Valeria aliamua kufuata Uislamu kama imani yake ya kidini na alichagua jina la Iman (imani).

Mnamo 1981 alihamia Damascus na kwa msaada wa mumewe na kikundi cha wanazuoni wa Syria, alifaulu kutafsiri Qur'ani kwa Kirusi mnamo 1991. Aliwasilisha kazi yake kwa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini. Sheikh Gad al-Haq Ali Gad al-Haq, ambaye wakati huo alikuwa Imamu mkuu wa kituo hicho chenye hadhi ya Misri, alianzisha kamati iliyojumuisha wataalamu wa Kirusi na Kiarabu kuchunguza tafsiri hiyo. Kamati hiyo ilisifu ubora wa kazi hiyo na Zayed bin Sultan Al Nahyan, Rais wa zamani wa Umoja wa Falme za Kiarabu, akafadhili uchapishaji wa nakala 25,000 za tafsiri hiyo.

Porokhova alizingatia maana ya kina na dhana za Qur'ani. Msomaji katika Amazoni ameielezea kazi hiyo kama tafsiri hiyo ya Qur'ani ya Kirusi kuwa yenye mvuto na ya kishairi ambayo inahifadhi maana na inawashilisha ujumbe kwa njia inayofaa.

Tafsiri hiyo ya Porokhova ilishinda tuzo ya kitabu bora cha mwaka cha Russia mwaka wa 1998. Kulingana na waandishi na watafsiri mashuhuri wa Kirusi, kazi hiyo ilikuwa na fungu kubwa katika kutambulisha Qur'ani kwa watu wa Russia.

Iman Porokhova aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake mnamo Septemba 2, 2019, akiwa na umri wa miaka 79.

Mikhailo Yaqubovic, mfasiri wa Qur'ani Tukufu katika lugha ya Kiukreni, alisifu kazi ya Porokhova, akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba: “Tafsiri ya Porokhova ilikuwa kama cheche ambayo iliibua shauku ya Qur'ani katika maeneo yote ya Urusi baada ya kuanguka kwa Muungano wa Sovieti. Iman Porokhova alikuwa mfano wa kuigwa kwa watu wengi na alikuwa mwanamke pekee aliyetafsiri Qur'ani Tukufu kwa katika lugha za Kislavic."

captcha