IQNA

Wanazuoni Mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiislamu / 10

Historia ya Tarjuma na Tafsiri ya Qur'ani Tukufu eneo la Balkan

21:18 - December 11, 2022
Habari ID: 3476230
TEHRAN (IQNA) – Kusoma Qur'ani Tukufu katika lugha yake asili ya Kiarabu ni changamoto kwa Waislamu wengi katika nchi zisizo za Kiarabu. Watarjumi na wafasiri wamejaribu kurahisisha mambo kwa kuandika tarjuma na maelezo au tafsiri kwa lugha mbali mbali za dunia.

Hata hivyo hatua ya baadhi ya wanazuoni kupiga marufuku tarjuma za Qur'ani kuliwahi kuleta changamoto kubwa kwa jamii za Waislamu wasio Waarabu.

Waislamu katika nchi za eneo la Balkan barani Ulaya (nchi kama vile Albania, Bosnia na Herzegovina, Bulgaria, Kroatia, Kosovo, Montenegro, Macedonia Kaskazini, Romania, Serbia, na Slovenia) walirithi mila ya Kiislamu ya Waothmania, na moja ya mila hizo ilikuwa ni marufuku ya kuandika tarujuma ya Qur'ani Tukufu.

Mnamo 1924 Mufti wa Albania alitangaza kuwa ni marufuku kwa Waislamu kusoma tarjuma za Qur'an na kwamba wanapaswa kusoma kitabu hicho kitakatifu kwa lugha yake asili ya Kiarabu.. Hii ilikuwa wakati Waislamu wengi wa Albania hawakujua Kiarabu.

Msimamo huu mkali ulipungua kidogo kidogo na mnamo 1937, tafsiri ya kwanza ya Qur'ani katika nchi za Balkan ilichapishwa huko Sarajevo na wanazuoni wawili maarufu wa Kiislamu walioitwa Muhamed Pandza na Dzemaludin Causevic.

Baada ya hapo, kizazi kipya cha watarjumi kilitayarisha tarjuma kumi zaidi za Qur'ani Tukufu.

Huko Albania, pia, mwanauzalendo anayeitwa Ilo Mitke Qafezezi alitayarisha tarjuma ya Qur'ani Tukufu  kutoka tarjumaa Kiingereza na kuchapisha sehemu ya kwanza mwaka wa 1921. Alisema lengo lake lilikuwa kuwaleta Waalbania Waislamu karibu na ndugu zao Wakristo. Alitaka pia Wakristo wapate kuisoma Qur'ani Tukufu.

Katika tafsiri yake, Qafezezi alijaribu kubaki mwaminifu kwa maandishi ya Qur'an iwezekanavyo. Mwishoni mwa miaka ya 1920 na 1930 uandishi wa tarjuma za Qur'ani uliendelea hadi chama cha kikomunisti kilipoingia madarakani na kuzuia kazi hiyo hadi 1991.

Baada ya marufuku ya tarjuma za Qur'ani Tukufu kuondolewa katika nchi za Balkan, wafasiri na wanafasihi walianza uandishi wa tarjuma za Kitabu hicho Kitakatifu.

Kilichotoa msukumo kwa mwelekeo huu miongoni mwa makabila mawili yenye Waislamu wengi katika nchi za Balkan (Waalbania na Wabosnia) ni ukweli kwamba wasio Waislamu walikuwa wameitarjumi Qur'ani Tukufu kwa misukumo ya utaifa.

Kwa mfano, tarjuma ya kwanza ya Qur'an ya Kiserbia ya Mico Ljubibratic (1829-1889) ambayo ilichapishwa baada ya kifo chake mwaka 1895 ililenga kuwavutia Waislamu wa Bosnia kuelekea katika mismamo ya kitaifa.

captcha