IQNA

Wanazuoni Mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiislamu / 8

Juhudi za Mwanazuoni wa Kimisri za Kufafanua juu ya Hadhi ya Wanawake katika Qur'ani

16:11 - November 30, 2022
Habari ID: 3476171
TEHRAN (IQNA) – Dkt. Fawzia al-Ashmawi alikuwa mwanazuoni ambaye alitumia maisha yake kueleza na kufafanua kuhusu hadhi ya wanawake katika Qur'ani Tukufu.

Al-Ashmawi, ambaye alifariki mwezi uliopita, alikuwa msomi wa Misri, mwandishi, mfasiri na mtarjumi. Alifanya kazi kama Profesa wa fasihi ya Kiarabu na ustaarabu wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Geneva. Pia aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Mambo ya Kiislamu, lenye uhusiano na Wizara ya Wakfu ya Misri, na mshauri wa UNSECO.

Alikuwa miongoni mwa wanachuoni waliozingatia mitazamo ya kisasa katika hotuba za kidini na alifanya utafiti kuhusu  Qur'ani, umuhimu wa akili katika kufasiri Uislamu kwa ujumla na hasa Qur'ani Tukufu, na pia hadhi ya juu ya wanawake katika Uislamu na jamii za Kiislamu, hususan nchini Misri.

Fawzia al-Ashmawi alizaliwa Alexandria, Misri, mapema miaka ya 1940. Alienda shule ya kimsingi ya Kikatoliki  na baada ya shule ya upili alijiunga na Chuo Kikuu cha Alexandria ambako alisoma katika Idara ya Lugha ya Kifaransa katika Kitivo cha Sanaa, ambako alihitimu mwaka wa 1965.

Al-Ashmawi kisha akaelekea Uswizi na kuendelea na masomo yake katika sayansi ya jamii huko hadi alipohitimu kutoka Kitivo cha Sanaa katika Chuo Kikuu cha Geneva. Akiendelea na masomo yake, alipokea Shahada ya Uzamili au MA mnamo 1974, na Shahada ya Uzamivu au PhD yake mnamo 1983 katika Sanaa, Binadamu na Sayansi ya Jamii. Tasnifu yake ya MA ilihusu haiba ya Mtume Muhammad (SAW) katika Fasihi ya Kifaransa, wakati tasnifu yake ya PhD ilikuwa Mwanamke na Misri ya Kisasa katika Kazi ya Naguib Mahfouz.

Al-Ashmawi alifanya kazi kama mtarjumi na mshauri katika baadhi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Uswizi, na ISESCO na UNESCO. Pia alifanya kazi kama mshauri wa kitamaduni katika Ubalozi wa Saudi Arabia, kisha katika Ubalozi Falme za Kiarabu huko Geneva. Alipandishwa cheo kutoka wadhifa wa profesa msaidizi na kuwa Mkuu wa Idara ya Lugha ya Kiarabu na Mafunzo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Geneva.

Msomi huyo mashuhuri alifariki mjini Geneva mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 80.

Kazi yake kuu ilikuwa "Mwanamke katika Qur'ani".  Katika kitabu hiki, anabainisha kwamba alipokuwa Makka, Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) alikabiliwa na upinzani mkubwa wa makafiri. Katika kipindi hiki, aya za Qur'ani zilikuwa zikitambulisha imani ya Mwenyezi Mungu mmoja kwa watu na kuwaita kwenye Uislamu. Katika zama hizi, mwanamke hakuwa na nafasi kubwa katika jamii na katika Sura za Makki, mwanamke alifunikwa na mwanaume. Katika Sura hizi, ni baadhi tu ya wanawake kama wake za mitume au mke wa Firauni wametajwa.

Lakini baada ya Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kuhamia Madina, tunaona jamii tofauti huko ambayo ina wingi wa kitamaduni. Hapa aya za Quran zinaweka wanawake kando ya wanaume. Katika sura zilizoteremka Madina, Muminat (waumini wanawake) na Muslimat (wanawake wa Kiislamu) wametajwa kando ya Muminin (waumini wa kiume) na Muslimin (wanaume Waislamu).

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha