IQNA

Nchi za Kiislamu zajadili masuala ya uwekezaji mjini Jeddah

13:29 - December 28, 2022
Habari ID: 3476321
TEHRAN (IQNA) - Warsha ilifanyika hivi karibuni huko Jeddah, Saudia kuhusu uwekaji wa huduma za kidigitali katika mashirika ya ustawishaji uwekezaji katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Warsha hiyo iliandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IDB) na Kituo cha Kiislamu cha Maendeleo ya Biashara (ICDT).

Katika  warsha ya siku mbili, maafisa wakuu 32 kutoka Mashirika ya Ustawishaji Uwekezaji (IPAs) katika nchi 29 wanachama wa IDB walishiriki, walishughulikia vipengele vya kiufundi vya kuimarisha uwekezaji wa kidijitali kupitia kubadilishana ujuzi, uzoefu na mbinu bora.

Warsha hiyo iliwafahamisha washiriki kuhusu manufaa ya kutumia teknolojia za kidijitali, vipengele muhimu vya mafanikio ya mabadiliko ya kidijitali katika kukuza uwekezaji na changamoto zinazokabili uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni.

Washiriki pia waliweza kubadilishana mawazo kuhusu nafasi tendaji ya uongozi wa taasisi za maendeleo za kimataifa, kama vile Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo; Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Kitakwimu, Kiuchumi na Kijamii kwa Nchi za Kiislamu; Shirika la Kiislamu la Bima ya Uwekezaji na Mikopo ya Mauzo ya Nje; Kamati ya Kudumu ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Kibiashara; Ofisi ya Uratibu na Jumuiya ya Biashara ya Kiislamu.

Warsha hiyo pia ilijadili ripoti ya kwanza ya pamoja ya mwaka ya IDB na ICDT kuhusu mazingira ya uwekezaji na fursa katika nchi za OIC.

Ripoti ya 2022 ilitoa takwimu na maelezo muhimu kuhusiana na uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni katika nchi za OIC ili kusaidia kutathmini mazingira ya uwekezaji, kuchanganua mwelekeo mkuu wa uwekezaji, kutambua masuala na kuunda sera za siku zijazo.

Washiriki walihitimisha warsha hiyo kwa mapendekezo ya kuandaa mpango kazi unaojumuisha shughuli za kuwezesha utekelezaji wa ramani ya mabadiliko ya kidijitali, inayolenga kukuza maendeleo ya uwekezaji wa sekta binafsi.

captcha