Katika matamshi yaliyotolewa mjini Tehran kabla ya safari hiyo, Rais Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya nchi za Kiislamu ili kukabiliana na njama za nje.
"Mikutano ya ngazi hii, kwa lengo la kukuza uhusiano wa karibu kati ya nchi za Kiislamu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, na kijamii, na kuwezesha kubadilishana uzoefu, ina ufanisi mkubwa," alisema.
Ameashiria nafasi muhimu ya Misri katika ulimwengu wa Kiislamu, akiielezea kama "nchi yenye historia ndefu na ustaarabu mkubwa ambayo ina jukumu kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu."
Rais amesisitiza umuhimu wa kujenga uhusiano wenye nguvu zaidi ndani ya ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza, "Kadiri uhusiano wetu na nchi za Kiislamu unavyozidi kuwa wa karibu, wa kina na wa kivitendo, ndivyo tunavyoweza kuzuia njama za maadui dhidi yetu na mataifa mengine ya Kiislamu kwa ufanisi zaidi."
Pia alibainisha kuwa majadiliano wakati wa mkutano huo yatajumuisha masuala muhimu yanayohusu Gaza, Palestina na Lebanon.
Mazungumzo hayo yanalenga kuchunguza njia ambazo nchi za Kiislamu zinaweza kuchukua msimamo mmoja wa kutetea haki za watu wanaodhulumiwa huko Gaza, Lebanon na Syria.
"Nchi za Kiislamu zinapaswa kimsingi kutumika kama waungaji mkono wa kila mmoja. Popote inapowezekana, tunapaswa kutatua tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo," Rais wa Iran alisema. "Mkutano huu unatoa fursa muhimu kwetu kuleta mitazamo yetu karibu na kuongeza ushawishi wetu wa kidiplomasia katika kanda," alihitimisha.
Ziara hiyo ni ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja kwa rais wa Iran kusafiri kwenda Misri. Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umedorora kwa muda mrefu.
Mahmoud Ahmadinejad alikuwa rais wa mwisho wa Iran kuzuru Misri mwezi Februari 2013 kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
D-8, au Nchi Nane Zinazoendelea, ni shirika la ushirikiano wa kiuchumi lililoanzishwa mwaka wa 1997 kupitia Azimio la Istanbul la Mkutano wa Wakuu wa Nchi.
Nchi wanachama wake ni pamoja na Iran, Uturuki, Pakistan, Bangladesh, Indonesia, Malaysia, Misri, na Nigeria.
Shirika linalenga katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kukuza maendeleo, na kukuza maslahi ya pamoja kati ya wanachama wake.
4254958