IQNA

Iran na Mauritani

Rais wa Mauritania apongeza misimamo imara ya Iran kuhusu Ulimwengu wa Kiislamu

20:38 - January 08, 2023
Habari ID: 3476374
TEHRAN (IQNA)- Rais Mohamed Ould Ghazouani wa Mauritania amepongeza misimamo thabiti na ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Ould Ghazouani ametoa pongezi hizo katika mazungumzo na Mohammad Mehdi Esmaili, Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran.
Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran, yuko Nouakchott, mji mkuu wa Mauritania, kuhudhuria hafla ya kuchaguliwa mji huo kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu.
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Nchi za Kiislamu (ISESCO) lililo chini ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC limechagua Nouakchott kuwa mji mkuu wa kitamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa mwaka huu wa 2023.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Rais wa Mauritania amesema katika mazungumzo hayo na Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran ya kwamba, kustawishwa uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kati ya nchi mbili za Magharibi mwa Asia na Kaskazini mwa Afrika kutakuwa na umuhimu na kwa manufaa ya kimkakati.

Ghazouani aidha ameeleza nia yake ya kuzuru Tehran na akashukuru mwaliko aliopewa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyyed Ebrahim Raisi.

Katika mazungumzo hayo Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran, Mohammad Mehdi Esmaili amesema mahusiano ya kiutamaduni na Ulimwengu wa Kiislamu na nchi za Kiafrika yameongezeka katika serikali ya 13 ya Iran na kwamba kukutana na kushauriana na mawaziri wa utamaduni wa nchi za Kiislamu kando ya hafla ya kuchaguliwa mji mkuu wa kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu ni fursa nzuri zaidi ya kuimarishwa mahusiano ya kiutamaduni kati ya Iran na nchi zingine za Kiislamu.
Katika safari yake hiyo nchini Mauritania, Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran amekutana pia na idadi kadhaa ya mawaziri wa nchi mwenyeji na mawaziri wa utamaduni wa nchi za Kiislamu waliohudhuria mkutano huo wa kuitambulisha Nouakchott kama mji mkuu wa kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu na kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali ya kiutamaduni ikiwemo kuwatambulisha wasanii wa nchi za Kiislamu, kuandaa makongamano ya kisanaa na kubadilishana athari za kiutamaduni na sanaa.

3704466

Kishikizo: mauritania iran isesco
captcha