IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Ufalme Bahrain wazuia maandamani ya kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

15:23 - January 28, 2023
Habari ID: 3476476
TEHRAN (IQNA) - Kundi kuu la upinzani nchini Bahrain, Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya al-Wefaq, limelaani utawala unaotawala wa kifalme wa ukoo wa Al Khalifa kwa kuwazuia Waislamu kufanya maandamano ya kupinga kuvunjiwa heshima Qur'ani barani Ulaya.

Siku ya Ijumaa, vikosi vya usalama vya Bahrain viliwakamata makumi ya raia waliokuwa wakienda kufanya maandamano hayo.

Pia walifunga njia zote za kuelekea Kituo cha Bait al-Quran karibu na ubalozi wa Uswidi ambako maandamano yalikuwa yamepangwa yafanyike.

Hatimaye waandamanaji walikusanyika  mahali pengine kwa ajili ya maandamano hayo.

Hussein al-Daihi, naibu katibu mkuu wa kundi hilo, katika taarifa yake ameitaja hatua hiyo kuwa ya fedheha na ya kulaumiwa, akisema inaonyesha hali ya ukandamizaji wa fikra katika utawala huo.

Amesema nara bandia za  kustahamiliana kidini ni njama inayotumiwa kujikurubisha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, utawala wa Manama ndio adui mkubwa wa uhuru wa kujieleza.

Wananchi wamefanya maandamano makubwa katika nchi kadhaa za Kiislamu duniani kote siku ya Ijumaa, kulaani matukio ya kuvunjiwa heshima kwa Qur'ani Tukufu barani Ulaya.

Jumamosi iliyopita Rasmus Paludan, mwanasiasa mwenye misimamo mikali wa Denmark alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm huku akiwa analindwa na polisi ya Uswidi. 

Aidha siku ya Jumapili, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.

Vitendo hivi vinaendelea kulaaniwa vikali na Waislamu pamoja na nchi za Kiislamu duniani ambapo serikali za Sweden na Uholanzi zimekosolewa kwa kuunga mkono vitendo hivyo viovu.

4117683

captcha