IQNA

Wasomi wa Afrika Kusini

Kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu ni kitendo cha kuhuzunisha na kinapaswa kulaaniwa

16:02 - January 30, 2023
Habari ID: 3476486
TEHRAN (IQNA) – Wasomi wa Afrika Kusini wamesema vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu ambavyo vimeshuhudiwa barani Ulaya hivi karibuni vinapaswa kulaaniwa.

Lerato Mokoena, profesa katika kitivo cha theolojia na dini katika Chuo Kikuu cha Pretoria cha Afrika Kusini alisema hayo katika mahojiano na IQNA kando ya mazungumzo ya Kiislamu na Ukristo kati ya Iran na Afrika Kusini, ambayo yalifanyika hapa Tehran hivi karibuni.

Alisema mzizi wa vitendo kama hivyo pengine ni chuki na kutovumiliana, "ndiyo maana tunapaswa kuja pamoja (na kujaribu kukuza uelewano)".

Mokoena aliongeza kuwa dini inaweza kusaidia sana katika suala la uwiano wa kijamii.

Alipoulizwa kama hatua za kupinga Uislamu barani Ulaya zinatokana na chuki dhidi ya wageni au Xenophobia, alisema Xenophobia na chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia ni tofauti lakini zinaoana wakati fulani na zote zinapaswa kupigwa vita.

Aliongeza kuwa jamii zinapaswa kusaidiwa ili kuweza kujenga mahusiano na kupendana na kumuona Mwenyezi Mungu ndani ya mtu mwingine.

Kuhusu maelewano ya kidini katika nchi yake, alisema, “Tunavumiliana kwa kiasi kikubwa kwa sababu kwa asili sisi ni jamii yenye watu kutoka jamii, kaumu, dini au rangi mbali mbali na kwa hivyo hatuna matatizo mengi sana linapokuja suala la kutovumiliana kwa kidini nchini Afrika Kusini.”

Naye Rantoa Letsosa kutoka Chuo Kikuu cha Free State  ambayo alikuwa miongoni mwa wasomi wa Afrika Kusini waliohudhuria mazungumzo ya dini mbalimbali mjini Tehran amesema ni muhimu kusisitiza kwamba watu wanapaswa kupendana.

"Tunapaswa kuona kila mtu kama ndugu au dada mwenzetu na kuwa na uhusiano mzuri sana kati yetu," alisema, na kuongeza kwamba jambo lolote baya kuhusu watu wengine ni jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa kamwe.

Alisisitiza kuwa Xenophobia na kuwachukulia watu wengine kama wageni ni jambo lisilokubalika.

"Nchini Afrika Kusini tuna matatizo kama haya yanayohusiana na Xenophobia lakini ni jambo ambalo tunapambana nalo na tunaamini kwamba watu wote wanapaswa kutendewa kwa utu na heshima."

Kuhusu matukio ya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu, amesema kuvunjia heshima na kudhalilisha matukufu ya dini nyengine kamwe ni jambo ambalo haipaswi kutokea.

Alisema watu wa dini tofauti wanapaswa kuzungumza wao kwa wao ili kuondoa hali ya kutoelewana. "Imani yangu ni kwamba tunapaswa kuishi kwa upendo na kwa heshima."

Akizungumzia nchi yake, alisema, “Siwezi kusema kuna masuala ya kidini nchini Afrika Kusini. Sisi ni jamii ya watu wa makabila, jamii, kaumu na dini mbali mbali na hivyo dini zinaheshimiwa. Hatujapata mizozo ya kidini nchini Afrika Kusini na nukta hii  ni chanya kabisa."

Mwanazuoni mwingine wa Afrika Kusini aliyezungumza na IQNA ni Profesa Maniraj Sukdaven wa Chuo Kikuu cha Pretoria ambaye alisema kuvunjia heshima matukufu ya kidini hufanywa ni baadhi ya nchi kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza lakini katika nchi nyingine ni chukizo kudhalilisha vitabu vya dini hususan Qur'ani Tukufu.

“Ikiwa unataka kuheshimu na kuelewa dini nyingine, kwa nini uchome vitabu vitakatifu? Nadhani ni makosa kwa maana hiyo kwa mtu yeyote kuchoma kitabu chochote kitakatifu. Ni makosa,” alisisitiza.

Pia alisema kwamba ni wenye itikadi kali katika jamii wanaochochea vurugu, “jambo ambalo ni kosa kabisa.”

Kwingineko katika matamshi yake, Profesa Sukdaven alisema kuna uhusiano mzuri kati ya dini zote nchini Afrika Kusini.

"Tuna maelewano mazuri (miongoni mwa dini) na tunakuza mazungumzo kati ya dini mbalimbali," alisema. "Idara yetu yenyewe itafanya kongamano la mazungumzo ya kidini. Nilipokuwa Chuo Kikuu cha Free State, nilianzisha jukwaa la mazungumzo kati ya dini mbalimbali ambalo bado lipo hadi leo na tuna dini kumi na mbili zinazokuja pamoja na kuzungumza ili kuelewana zaidi, kujifunza kuhusu kila mmoja na kukubali kila mmoja kwa kile ambacho kila mtu anaamini.

3482273

Habari zinazohusiana
captcha