IQNA

Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

Sheikh Naim Qassem: Kuvunjiwa heshima Qur'ani ni ishara ya kufilisika kimaadili kwa nchi za Magharibi

17:32 - February 01, 2023
Habari ID: 3476498
TEHRAN (IQNA)- Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika baadhi ya nchi za Magharibi, vitendo vya kigaidi na kuuawa Waislamu huko Pakistan ni ishara ya kufilisika nchi za Magharibi.

Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, kuvunjiwa heshima kwa makusudi Qur'ani Tukufu huko Sweden, Uholanzi na baadhi ya nchi za Magharibi chini ya usimamizi wa serikali za nchi hizo kunaonyesha kiwango kikubwa cha dhulma na uchokozi dhidi ya Waislamu ambao hawakubali kupotoshwa na upotofu na fikra za Kimagharibi.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa, kusadifiana kwa kitendo cha nchi za Magharibi cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu na hatua ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh linaloungwa mkono na Marekani ya kuua mamia ya watu nchini Pakistan ni ishara ya kufilisika kwao katika ngazi ya ubinadamu.

Hapo awali, harakati ya Hizbullah ya Lebanon ilikuwa imetangaza katika taarifa yake ya salamu za rambirambi kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Waislamu wasiopungua mia moja msikitini nchini Pakistan, kwamba sera ya makundi ya kitakfiri ya kuendelea kufanya jinai za kutisha na kulenga usalama na utulivu wa nchi za Kiislamu inazidisha udharura wa kuwepo ushirikiano kati ya nchi za Kiislamu ili kupambana na wauaji ambao wanajivika vazi la dini. 

Matamshi ya Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah yametolewa baada ya kundi la kitakfiri kuua Waislamu wasiopungua mia moja waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala msikini katika mji wa Peshawar huko kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Vilevile yanafuatia hatua ya baadhi ya wanasiasa wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia katika nchi za Ulaya ya kuchoma moto na kurarua nakala za kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

4118756

captcha