IQNA

Mazungumzo ya kidini

Mkuu wa ICRO: Vitendo vya kuvunjia heshima matukufu ya kidini vinaratibiwa

18:44 - January 29, 2023
Habari ID: 3476484
TEHRAN (IQNA) – Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO) amesema kurudiwa kwa kesi za kuvunjia heshima matukufu ya kidini na ukimya au uhalalishaji unaofanywa na serikali za Magharibi kwa jina la uhuru wa kujieleza unaonyesha mwelekeo wa kimfumo wa kueneza chuki.

Hujjatul Islam Mohammad Mehdi Imanipour aliyasema hayo alipokuwa akihutubia katika mazungumzo ya pili ya dini  za Kiislamu na Ukristo kati ya Iran na Afrika Kusini, yaliyoanza mjini Tehran siku ya Jumamosi.

Hata hivyo, amesema, inatarajiwa kwamba wenye mapenzi mema watatoa jibu linalofaa katika kukabiliana na vitendo hivyo ili kuzuia kuumiza hisia za watu wa dini na madhara kwa maadili.

Matamshi yake yametolewa baada ya visa kadhaa vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika baadhi ya nchi za Ulaya.

Wiki iliyopita Rasmus Paludan, mwanasiasa mwenye misimamo mikali wa Denmark alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm huku akiwa analindwa na polisi ya Uswidi. 

Aidha wiki iliyopita pia, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.

Vitendo hivi vinaendelea kulaaniwa vikali na Waislamu pamoja na nchi za Kiislamu duniani ambapo serikali za Sweden na Uholanzi zimekosolewa kwa kuunga mkono vitendo hivyo viovu.

Kwingineko katika matamshi yake, Hujjatul Islam Imanipour alisema maadili yameathiriwa katika jamii katika ulimwengu wa sasa, na kuongeza kuwa kuna haja ya mijadala zaidi ya dini mbalimbali kuhusu mada ya maadili katika dini.

Alisema katika mfumo wa kimaadili wa Uislamu, lengo kuu la tabia za kimaadili ni kufikia ukamilifu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba wa kila kitu na chimbuko la maadili yote.

Mazungumzo ya pili ya kidini kati ya Uislamu na Ukristo kati ya Iran na Afrika Kusini yanafanyika katika Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO) mjini Tehran huku mada kuu ikiwa ni  "Maadili katika Dini" kwa kushirikisha wasomi na wanafikra kutoka nchi hizo mbili.

Repetition of Insulting Religious Sanctities Sign of Systemic Hate-Mongering: ICRO Chief

4117723

captcha