“Ujumbe mkuu wa matembezi ya Arbaeen ni mwangaza. Leo, kama ilivyokuwa daima, yanatoa ujumbe wa uthabiti, muqawama, kujitolea, na mwangaza, yakisimama kama jibu la kivitendo kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu," amesema Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO), Hujjatul-Islam Mohammad Mehdi Imanipour.
Aliyasema haya alipokuwa akihutubia hafla ya kufunga Tuzo ya 10 ya Kimataifa ya Arbaeen, iliyofanyika Tehran Jumatano asubuhi.
Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia siku ya arobaini baada ya Siku ya Ashura, ambayo ni siku ya kukumbuka kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imamu wa tatu wa Shia.
Ni moja ya mjumujo mkubwa zaidi wa kidini wa kila mwaka ulimwenguni, ambapo mamilioni ya Waislamu, aghalabu wakiwa wa madhehebu ya Shia hutembea kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jiran pamoja na kona zote za dunia.
“Imam Hussein (AS) si wa itikadi yoyote maalum; yeye ni shakhsia wa ubinadamu,” alisema Imanipour.
“Lengo la maandamano ya Arbaeen ni kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu,” aliongeza, “Yanahudumu kama jukwaa la njia ya maisha ya Kiislamu, yakionyesha roho adhimu ya kusaidiana, udugu, na maisha yenye imani. Yanachochea hisia za kina za umaanawi na kuonyesha njia ya maisha ambayo imewatia hofu maadui.”
“Tumeona kuwa matukio madogo mara nyingi hupata kuakisiwa na kupigiwa debe sana kimataifa, ilhali kumekuwa na kimya kikubwa kuhusu Arbaeen,” alisema msomi huyo wa Kiislamu.
Wakati vyombo vingine vya habari vinavyotafuta uhuru vimeweza kutoa taarifa nzuri kuhusu tukio hili, bado kuna njama ya makusudi ya ukimya na kubana habari kuhusu tukio hili, aliongeza.
“Wakati wapinzani waliposhindwa kuukubali mfumo huu wa maisha ya imani, walikimbilia upotoshaji, wakidai kwa uongo kuwa ni mpango unaodhaminiwa na serikali, ilhali kimsingi umejikita mioyoni mwa watu na juhudi zao binafsi,” alisema Hujjatul Islam Imanipour.
3491470