IQNA

Mapinduzi ya Kiislamu

Katibu Mkuu wa Jihad Islami ampongeza Kiongozi Muadhamu kwa mnasaba wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

22:58 - February 12, 2023
Habari ID: 3476551
TEHRAN(IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Ziyad al-Nakhalah amemtumia ujumbe Kiongozi Muadhamu wa Mapiinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei akimpongeza kwa mnasaba wa kutimia miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Al-Nakhalah amesisitiza katika ujumbe wake kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu yalibadilisha sura ya eneo la Magharibi mwa Asia na kuacha taathira kubwa duniani kote sambamba na kuathiri sera na siasa za dunia. Amesisitiza kuwa:"Kutokana na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, haki ilipata anwani yake, wapigania uhuru wakapata nguzo na kimbilio, na kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipeperusha bendera ya watu wote wanaopigania uhuru.

Katibu Mkuu wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema katika ujumbe wake kwamba: Mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa nguzo imara na muungaji mkono mkubwa kwa wananchi wa Palestina wanaopigana Jihadi na wanaoendelea kudhulumiwa na kuongeza kuwa: "Taifa letu la Palestina na mapambano yake ya ukombozii yameimarika zaidi hii leo kuliko wakati mwingine wowote, licha ya changamoto zote na licha ya uungaji mkono na msaada ambao adui wa Kizayuni anaupata kutoka Marekani na Magharibi.

Ziyad al-Nakhalah ameendelea kusema: "Hii leo tunakaribia ushindi, Mwenyezi Mungu akipenda. Licha ya kuzingirwa na mabeberu, mujahidina wetu katika ardhi yote ya Palestina, wanaonyesha ushujaa katika makabiliano yao na vikosi vya Wazayuni." Amesisitiza kuwa viongozi wa utawala ghasibu wa Israel sasa wanazungumza kwa wasiwasi juu ya uwezekano wa kuangamizwa na kutoweka utawala huo.

Mamilioni ya Wairani jana walishiriki katika sherehe za ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ili kusisitiza tena mshikamano wao mkubwa, kizazi baada ya kizazi, na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, wakipeperusha bendera ya Uislamu na kuzidisha matumaini ya kupata ushindi watu wote wanaokandamizwa na kudhulumiwa duniani.

Sherehe za mwaka huu za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran zilikuwa na ladha ya kipekee, hasa baada ya kufeli njama kubwa iliyoanzishwa na madola ya kigeni dhidi ya Iran ya Kiislamu katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, iliyolenga usalama wa ndani na umoja na mshikamano wa taifa kwa kuibua ghasia na kuziunga mkono kupitia vita mseto vya kisiasa, kiuchumi na hujuma ya vyombo vya habari vya Magharibi. Hata hivyo hujuma na vita hivyo vilishindwa kutokana na mwamko, umakini, kusimama kidete, umoja na mshikamano wa wananchi na hekima ya viongozi wao.

 

3482446

captcha