IQNA

Mwaka wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Raisi: Adui hawezi kustahamili ustawi na hatua ilizopiga Iran

17:31 - February 11, 2023
Habari ID: 3476543
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusiana na mafanikio yaliyopatikana nchini katika nyuga mbalimbali za sayansi, teknolojia, uchumi, ulinzi, afya na tiba kwamba adui hawezi kuyavumilia maendeleo na hatua ilizopiga Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo mbele ya hadhara ya umati mkubwa wa wananchi waliohudhuria maadhimisho ya mwaka wa 44 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, maarufu kama shehre za 22 Bahman (11 Februari) yaliyofanyika kwenye mzunguko wa mnara wa Azadi hapa mjini Tehran na akabainisha kuwa, licha ya vitisho na vikwazo mbalimbali, leo hii Iran ya Kiislamu imefanikiwa katika vielezo vya ukuaji thabiti wa mitaji, ukuaji wa kiwango cha uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ukuaji wa vielezo vingine.

Seyyid Ebrahim Raisi ameongeza kuwa, maadui walipoona Iran inazidi kupiga hatua mbele katika nyanja zote na haijasita, walianzisha njama nyingine na kudhani kwamba wanaweza kuisimamisha nchi kwa fujo na machafuko, lakini wameshindwa tena.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kueleza kwamba, leo ni siku ya kudhihirisha umoja na mshikamano wa kitaifa na kushiriki katika hamasa ya upazaji sauti ya umma na akasisitiza kwamba, wale waliotekwa na hila za adui katika machafuko ya hivi karibuni wajue kuwa, wananchi wenzao wa Iran wanawapokea kwa mikono miwili na kwamba serikali ya 13 itaendeleza serikalini na katika vyombo vya uendeshaji mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa kuyachukulia mambo kwa jicho la baba mzazi.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Raisi amesema, wananchi wa Iran wametambua kuwa adui hajashughulishwa na suala la mwanamke, uhuru, maisha na haki za binadamu; na akafafanua kwa kusema, anachofuatilia adui ni kulinyang'anya taifa la Iran uhuru, kujitawala na maisha ya watu wake; na wananchi wa Iran wanaelewa vyema kwamba, maadui hao hawakuwapa hayo maisha watu wa Afghanistan, Iraq, Lebanon na Syria hata watake kufanya hivyo kwa Wairani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu, leo wanawake wa Kiirani wanashiriki kwa wingi katika nyanja za kielimu, kisiasa, kijamii na kiuchumi na akawahutubu Wamagharibi: "kuhusiana na haki za wanawake, sisi ni wa kuwahoji nyinyi na nyinyi ni watuhumiwa, kwa sababu mnawatumia wanawake kibidhaa kwa ajili ya kujipatia faida zaidi".

Aidha, Seyyid Ebrahim Raisi amebainisha majonzi na masikitiko yake kwa watu walioathiriwa na tetemeko la ardhi katika nchi za Uturuki na Syria na akasema, Iran ni msaidizi wa majirani wote katika siku za shida na adui ajue kwamba, amekosea sana kama anadhani atapata nafasi katika eneo hili, kwa sababu kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amani na usalama wa eneo umefungamana na kuondoka Marekani na waitifaki wake.

4121290

Habari zinazohusiana
captcha