IQNA

Azimio la Bahman 22

Mshikamano na umoja wa kitaifa ni mkakati muhimu kwa ajili ya kumsabaratisha adui

17:38 - February 11, 2023
Habari ID: 3476544
TEHRAN (IQNA)- Wananchi wa Iran wametangaza katika azimio lao walilotoa mwishoni mwa maandamano ya Bahman 22 ya kwamba, kuwa kitu kimoja, kuungana, mshikamano, umoja wa kitaifa, kuwa na moyo mmoja makundi na matabaka na kushirikiana watu wa kaumu na dini zote nchini ni wajibu wa kidini na kimapinduzi na ndio mkakati muhimu zaidi wa kumshindia adui.

Katika azimio lililotolewa mwishoni mwa maandamano ya Bahman 22 ya kuadhimisha mwaka wa 44 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, taifa la Iran limewahutubu vinara wa ubeberu na wanaojidai kutetea uhuru wa imani na uhuru wa maoni, -ambao kutokana na hofu waliyonayo juu ya kuenea nuru ya Qur'ani wamelifanya suala la kuupiga vita Uislamu na kueneza chuki dhidi ya Uislamu mkakati wa uadui wao- ya kwamba, leo ukweli wa kitabu cha mbinguni cha Qur'ani umezidi kuwadhihirikia watu wa Magharibi wenye kiu ya maadili mema na umaanawi, ambao wamechochwa na nadharia zilizobuniwa na wanadamu.

Azimio hilo limeeleza kuwa, tokea zamani, wananchi wa Iran ya Kiislamu wana uelewa juu ya mtazamo kinzani, haribifu, wa udhalilishaji na wa ufuska wa utamaduni wa Magharibi kuhusiana na mwanamke, na matokeo ya kutisha ya mtazamo huo kwa ustawi na utukukaji wa wasichana na wanawake katika miundo tofauti ya kielimu, kisiasa, kijamii, kiutamduni na kimichezo; kwa hivyo linawataka viongozi husika nchini wachukue hatua zinazofaa ili kuzuia kutekelezwa njama chafu za adui na kuharibiwa heshima na tunu tukufu za wanawake wa Kiirani.

Azimio la Bahman 22 limeeleza bayana kuwa, leo kambi ya shetani ikiongozwa na Marekani mtenda jinai na utawala wa Kizayuni imeanzisha vita vikubwa na tata mno vya mchanganyiko, ambapo kwa kutumia mtandao wake wa ubeberu wa vyombo vya habari imedhamiria kuzihafifisha athari za kudumu za Mapinduzi; kwa hiyo wananchi wa Iran wanawataka wahusika wote katika uga wa fikra na utamaduni pamoja na makhatibu na waandishi kuuzingatia mkakati wa Jihadi ya Ubainishaji na kubanisha ukweli halisi wa tunu za utamaduni na thamani za Kiislamu ili kuzima njama chafu za adui.

Halikadhalika, katika azimio lao hilo, wananchi wa Iran wamesisitiza haki na ustahiki wa mhimili wa Muqawama na ulazima wa kuwatetea na kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, Lebanon, Syria na Yemen, sambamba na kupanuliwa wigo wa mkakati wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kupitia azimio lao hilo, wananchi wa Iran wameeleza pia kuwa wako pamoja na wananchi wenzao walioathiriwa na tetemko la ardhi katika mji wa Khui na vilevile wametoa mkono wa pole kufuatia tukio chungu la mtetemeko wa ardhi katika nchi za Uturuki na Syria na kuyataka mataifa na nchi zote hasa za Kiislamu kutekeleza jukumu lao la kiutu na Kiislamu la kuwasaidia waathirika ili kupunguza machungu na majonzi waliyonayo.

4121283

captcha