IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Uswidi yatoa waranti kukamatwa aliyevunjia heshima Qur'ani Tukufu

19:37 - May 06, 2023
Habari ID: 3476964
TEHRAN (IQNA)- Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Malmö nchini Uswidei (Sweden) imetoa waranti wa kukamatwa kwa mwanasiasa mwenye misimamo mikali wa Denmark mwenye asili ya Uswidei "Rasmus Paludan" ambaye hivi karibuni aliivunjia heshima Qur'ani Tukufu.

Rasmus Paludan, kinara wa kundi la mrengo mkali wa kulia nchini Denmark liitwalo Hard Line, mnamo Januari 21 na kwa msaada na ulinzi  wa polisi, alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na Ubalozi wa Uturuki huko Stockholm, Uswidi na siku chache baadaye, akazichoma moto nakala mbili za Qur'ani Tukufu mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Copenhagen, Denmark na karibu na msikiti.

Mwezi uliopita wa Aprili pia kundi la watu wenye misimamo ya chuki nchini Denmark limeivunjia heshima Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Uturuki mjini Copenhagen.

Kitendo hicho kiovu kilifanywa na mwanachama mmoja wa kundi lenye chuki na Uislamu na lenye mielekeo ya utaifa la Patrioterne Gar Live nchini Denmark mbele ya ubalozi wa Uturuki mjini Copenhagen.

Watu wengi wenye misimamo mikali ya chuki katika nchi za Ulaya hususan Denmark wameivunjia heshima Qur'ani Tukufu na kuzichoma moto nakala za Kitabu hicho cha mbinguni kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni, jambo ambalo limelaaniwa vikali na Waislamu kote duniani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani wimbi la kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Denmark na katika nchi nyingine za Ulaya.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali wimbi hilo la kuvunjiwa heshima Kitabu Kitukufu cha Waislamu katika nchi kadhaa za Ulaya na kueleza kuwa, vitendo hivyo vinahatarisha amani na utaratibu wa kuishi kwa utangamano jamii ya wanadamu.

Kan'ani amekosoa pia kimya cha wale wanaojinadi kuwa watetezi wa haki za binadamu duniani, kwa kufumbia macho vitendo hivyo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Amesema vitendo hivyo vinachochea misimamo mikali, ghasia na kuhatarisha usalama wa dunia.

3483438

captcha