IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Sheikh Zakzaky: Nchi za Kiislamu zisusie bidhaa za nchi zinazovunjia heshima Qur'ani Tukufu

15:34 - September 13, 2023
Habari ID: 3477594
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) amesema kuwa, kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu ni hujuma dhidi ya mataifa ya Kiislamu katika sehemu tofauti za dunia na ametaka mataifa ya Kiislamu yasusie bidhaa za nchi zinazoidhinisha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Katika mahojiano maalumu na ripota wa Iran Press mjini Abuja, Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, nchi za Kiislamu zinapaswa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya nchi yoyote ya Ulaya inayounga mkono vitendo vya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.

Akizungumzia sababu za kuchomwa moto nakala za Qur'ani barani Ulaya, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema, wamegundua kuwa Qur'ani Tukufu ndiyo ujumbe pekee wa Mwenyezi Mungu na imepewa kinga na kupotoshwa au kubadilishwa. Shekh Zakzaky amesisitiza kuwa, kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu ndio njia pekee ya kuokoa wanadamu wote.

Sheikh Ibrahim Zakzaky ameongeza kuwa, Wamagharibi wametambua jinsi Qur'ani Tukufu ilivyo muhimu kwa Waislamu, na kushikamana kwa Umma wa Kiislamu na kitabu hiki kitakatifu kuna maana kwamba, hakuna mtu anayeweza kuwabadilisha Waislamu, kwa sababu Qur'ani Tukufu haiwezi kubadilishwa.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuhusu hatua inayyopaswa kuchukuliwa na nchi za Kiislamu dhidi ya vitendo vya kuendelea kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika baadhi ya nchi za Ulaya kwamba, Umma wa Kiislamu na nchi za Kiislamu kwa ujumla zinapaswa kususia bidhaa za nchi zinazounga mkono vitendo hivyo viovu.

Sheikh "Ibrahim Zakzaky" amesema kuwa sheria inayokataza kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu inapaswa kuanzishwa katika nchi za Ulaya, na kuongeza kuwa: Wasipofanya hivyo watu watachukua hatua dhidi yao, kwa sababu Qur'ani Tukufu ni sehemu ya Waislamu.

3485154

Habari zinazohusiana
captcha